Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC juzi Jumapili walijiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea Rwanda baada ya kuisambaratisha KMKM ya Zanzibar kwa mabao 4-0. Ushindi huo umeifanya Azam kufikisha pointi nne baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Rayon Sports ya Rwanda kwenye mechi yao ya kwanza. Mabao ya Azam yalifungwa na John Bocco na Leonel Saint-Preux waliofunga mawili kila mmoja. Azam ambao walipewa tiketi ya kushiriki michuano hiyo baada ya Yanga kushindwa kukidhi matakwa ya Cecafa, leo Jumanne itacheza na Atlabara ya Sudani Kusini ikiwa ni mechi yao ya tatu katika michuano hiyo. Katika mechi ya Awali Telecom ya Djibout iliifunga KCCA ya Uganda mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi B. Rayon Sports walicheza na Coffee ya Ethiopia katika mchezo wa tatu wa Kundi A.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |