Uongozi wa Simba umeamua kumfukuza kazi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Zdravko Logarusic, lakini kocha huyo ameondoka na kitita cha Sh milioni 5 kwa muda wa wiki tatu pekee tangu aliposaini mkataba mpya klabuni hapo bila kufanya kazi yoyote ya maana. Logarusic amechukua kitita hicho akiwa ameiongoza Simba kwenye mechi moja tu ya kirafiki dhidi ya Zesco ya Zambia ndani ya muda huo ambapo Simba ililala kwa mabao 3-0. Mbali na fedha hizo alizoondoka nazo, kocha huyo aliiongoza Simba kushika nafasi ya pili ya Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu. Simba ilitinga fainali ya michuano hiyo ambapo ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya KCCA ya Uganda. Katika rekodi nyingine Logarusic aliiongoza Simba katika mechi 13 za Ligi Kuu Bara, Simba ilishinda mara tatu pekee. Ilipoteza michezo mitano na kutoka sare mitano na kumaliza nafasi ya nne. Logarusic aliikuta Simba katika nafasi hiyo hiyo ya nne wakati anakabidhiwa timu Desemba mwaka jana kwa mkataba wa kwanza.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |