• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Madaktari wa China washirikiana na wa Afrika kupambana na ugonjwa wa Ebola

    (GMT+08:00) 2014-08-15 16:38:44

    Nchi kadhaa za Afrika Magharibi zimekumbwa na ugonjwa wa Ebola. Huu ni mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa huo kutokea tangu virusi vya Ebola vigunduliwe mwaka 1976. Hivi sasa ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja. Nchini Sierra Leone, madaktari kutoka China wanashirikiana na wenzao waafrika kupambana na ugonjwa huo.

    Mkuu wa kikundi cha matibabu cha China nchini Sierra Leone Dr. Wang Yaoping amefahamisha kuwa kikundi chake chenye madaktari 10 kinafanya kazi katika hospitali ya King Harman Road mjini Freetown kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Tangu ugonjwa wa Ebola ulipuke mwezi Mei nchini humo, kazi na maisha ya madaktari wa China vimekuwa na changamoto kubwa. Dr. Wang anasema,

    "Baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, idadi ya wagonjwa wanaokuja katika hospitali yetu haijapungua, baadhi yao huenda waliwahi kwenda kwenye maeneo yenye maambukizi ya Ebola, au wanatoka kwenye maeneo hayo. Mwezi uliopita mgonjwa mmoja alikuja kwenye hospitali yetu, tulidhani ameambukizwa ugonjwa wa Ebola, na kuwaita wafanyakazi wa kituo cha kudhibiti maradhi kupima damu yake. Siku ya pili alithibitishwa kuwa mgonjwa wa Ebola. Tunakabiliwa na hatari kubwa."

    Kutokana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Ebola, baadhi ya nchi zimeondoa vikundi vya madaktari wao. Dr. Wang amesema kutokana na urafiki wa kindugu uliopo kati ya watu wa China na wa Afrika, na jukumu lililotolewa na serikali ya China, kikundi cha matibabu cha China kimeamua kushirikiana na ndugu wa Afrika kupambana na ugonjwa huo. Anasema,

    "Serikali ya China imetupa jukumu la kutoa msaada barani Afrika. Na tukiwa madaktari, tunapaswa kuwasaidia wagonjwa. Tunapokabiliwa na maafa makubwa na maambukizi ya magonjwa, tunapaswa kufanya kazi badala ya kukimbia."

    Tangu China ianze kutuma vikundi vya matibabu nchini Sierra Leone mwezi Machi mwaka 1973, kwa ujumla China imetuma vikundi 16 vyenye madaktari 212 nchini humo. Licha ya kikundi cha matibabu kinachoongozwa na Dr. Wang Yaoping, madaktari wengine wa China wanafanya kazi katika hospitali ya urafiki kati ya Sierra Leone na China iliyoko kilomita 20 kutoka Freetown. Naibu mkuu wa hospitali hiyo kutoka Sierra Leone Dr. Kanu amewachukua Wachina hao kuwa marafiki zake, akisema,

    "Wachina ni marafiki zetu hivyo wamebaki hapa kutusaidia. Nadhani hawatatuacha kutokana na ugonjwa wa Ebola, watashikilia kushirikiana nasi kupambana na ugonjwa huu."

    Hospitali ya urafiki kati ya Sierra Leone na China hivi karibuni ilimpokea mgonjwa wa Ebola, sasa madaktari 7 wa China waliokutana naye wametengwa ili kuchunguzwa kama wameambukizwa, na hospitali hiyo imefungwa kwa muda. Dr. Kanu amesema, baada ya muda wa kutengwa kwisha, hospitali hiyo itafunguliwa tena na kuendelea kupokea wagonjwa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako