• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Roboti zaanza kutumiwa katika viwanda nchini China

    (GMT+08:00) 2014-08-20 14:34:33

    Katika kampuni maarufu ya viyoyozi ya Gree iliyoko katika delta ya mto Changjiang nchini China, mashine mbalimbali zinatengeneza plastiki kuwa vipuri vya viyoyozi, mikono ya roboti inaweka vipuri kwenye mkanda wa kuchukulia, roboti zinapeleka vitu mbalimbali hapa na pale, na wafanyakazi wawili au watatu tu wanasimama mwisho wa sehemu ya kukagua na kuchukua bidhaa zilizokamilika kutengenezwa. Meneja mkuu wa kampuni ya Gree Bw. Dong Mingzhu amesema ndani ya miaka miwili ijayo, kampuni yake itatenga yuan bilioni 5 kujenga kiwanda ambacho asilimia 70 ya kazi zitafanywa na roboti, anasema,

    "Katika muda usiozidi miaka miwili, tutafanya mabadilikjo makubwa sana ya uzalishaji katika kampuni. Sasa kuna wafanyakazi wachache tu wanaofanya kazi kiwandani."

    Licha ya makampuni makubwa ya China ikiwemo kampuni ya Gree, makampuni mengi madogo na ya ukubwa wa kati pia yameanza kutumia roboti badala ya kuwaajiri wafanyakazi wengi. Kampuni ya teknolojia ya Rapoo inatengeneza vifaa vya kompyuta mjini Shenzhen. Mwaka 2012, mafundi wa kampuni hiyo wakiongozwa na naibu meneja mkuu Bw. Deng Qiuwei walisanifu mstari wa kuzalisha keyboard na mouse kwa roboti. Mfanyakazi mmoja anasema,

    "Roboti zinafanya kazi kwa kasi sana. Nadhani katika siku za baadaye roboti nyingi zaidi zitafanya kazi badala ya binadamu."

    Katika miaka miwili iliyopita, roboti zilichukua asilimia 75 ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, na gharama za kuwaajiri wafanyakazi zimepungua kwa yuan milioni 100 kwa mwaka. Bidhaa za kampuni hiyo zinauzwa vizuri katika soko la kimataifa kutokana na bei nafuu na sifa nzuri. Makampuni mengi yanashangazwa na mafanikio ya kampuni hiyo, na kuiomba kuzalisha roboti ili kukidhi mahitaji yao. Kutokana na ombi hilo, kampuni hiyo sasa imeanzisha kazi mpya ya kuzalisha roboti, na imepata orodha nyingi za uagizaji. Bw. Deng Qiuwei anasema,

    "Katika muda usiozidi mwaka mmoja, tumepata orodha za uagizaji kutoka makampuni ya uzalishaji zaidi ya kumi, zikiwemo simu za mkononi, GPS, mizani, adapta za umeme, na vifaa vingine mbalimbali vya umeme."

    Mkurugenzi wa idara ya kusukuma mbele uvumbuzi ya kampuni ya elektroniki ya DBG ya mkoa wa Guangdong Bw. Huang Fuxin anaridhika na roboti tatu za kuzungusha parafujo alizonunua, anasema,

    "Zamani mfanyakazi alihitaji dakika moja kuzungusha parafujo moja, sasa roboti inamaliza kazi hii kwa sekunde 40 tu. Tena roboti haiwezi kusahau kuzungusha parafujo hata moja, lakini mfanyakazi anaweza kusahau. Roboti ni kama mfanyakazi hodari asiyehitaji mafunzo."

    Roboti inaweza kuhakikisha sifa ya bidhaa, kuinua ufanisi na kupunguza gharama, hivyo makampuni mengi ya China yameanza kununua roboti. Katika hali hii, makampuni mengi ya uzalishaji wa roboti ya kimataifa ikiwemo kampuni ya ABB, yameanzisha matawi yao nchini China, na zaidi ya maeneo 30 ya viwanda vya uzalishaji wa roboti yameanzishwa nchini China. Kampuni maarufu ya kutengeneza mashine kubwa ya Sany imetenga fedha nyingi kushughulikia kazi hii, na kampuni ya makontena ya kimataifa ya China pia imeanza usanifu wa roboti, na kutarajia kuwa roboti zitafanya kazi badala ya asilimia 20 ya wafanyakazi.

    Katika miongo kadhaa iliyopita, shughuli za utengenezaji zilipata maendeleo ya kasi, na China imekuwa "kiwanda kikubwa zaidi duniani". Lakini katika miaka ya hivi karibuni, gharama ya nguvu kazi nchini China imepanda, na nguvu kazi yenye bei nafuu kutoka nchi za Asia Kusini Mashariki na India zimeleta shinikizo kubwa kwa makampuni ya China. Meneja mkuu wa kampuni ya roboti ya Siasun ya mji wa Shenyang ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya roboti nchini China Bw. Qu Daokui anaona kuwa, makampuni ya utengenezaji ya China yanatakiwa kutumia roboti ili kuongeza uwezo wa kushindana, akisema,

    "Hivi sasa uzalishaji kwa kutumia nguvu kazi nyingi unahamia katika nchi za Asia Kusini Mashariki, Mexico na India. China haina uwezo mkubwa wa kushindana katika uzalishaji wa aina hii kutokana na ukosefu na gharama kubwa ya nguvu kazi. Hivyo makampuni ya China yanatakiwa kuboresha shughuli zao kwa kutumia roboti."

    Mwishoni mwa mwaka jana, wizara ya viwanda na upashanaji habari ya China ilitoa waraka wa maoni kuhusu kusukuma mbele maendeleo ya uzalishaji wa roboti. Waraka huo unasema, ifikapo mwaka 2020, China itajenga mfumo kamili wa uzalishaji wa roboti, kuandaa makampuni matatu hadi matano ya uzalishaji wa roboti yenye uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa, kuinua uwezo wa uvumbuzi na ushindani wa makampuni ya uzalishaji wa roboti, kuchukua asilimia 45 ya soko la roboti za kiwango cha juu, na kuifanya idadi ya roboti ifikie 100 kwa kila wafanyakazi elfu 10.

    Takwimu zilizotolewa na shirikisho la kimataifa la roboti zinaonesha kuwa, mwaka jana roboti elfu 37 ziliuzwa katika soko la kimataifa, idadi ambayo ni karibu mara tatu ya ile ya mwaka 2012. Takwimu zilizotolewa na shirikisho la roboti la China pia zimethibitisha ongezeko la matumizi ya roboti. Naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Bw. Yao Zhiju alifahamisha kuwa, moja kati ya roboti tano zinazouzwa duniani inatumiwa nchini China, akisema,

    "Mwaka jana China imekuwa soko kubwa zaidi la roboti badala ya Japan. Ongezeko la matumizi ya roboti nchini China ni kubwa zaidi duniani."

    Ikilinganishwa na nchi zilizoendelea, China imechelewa kusanifu na kutumia roboti. Hivi sasa asilimia 90 ya roboti zinazouzwa katika soko la China zinazalishwa na makampuni ya nchi za nje. Usanifu na matumizi ya roboti vimetiliwa maanani na nchi nyingi duniani, makampuni ya China pia yanafanya juhudi kushughulikia kazi hii. Kampuni ya roboti ya Siasun ya mjini Shenyang ni moja kati ya makampuni hayo. Ukiingia kiwanda kipya cha kampuni hiyo, utajiona kama uko katika kiwanda cha miaka ijayo. Meneja mkuu Qu Daogui anasema,

    "Kiwanda hiki ni cha kisasa zaidi duniani, roboti zinazalisha roboti hapa."

    Aina mpya ya roboti ambazo zinaweza kutembea bila ya betri au kuunganishwa na waya wa umeme, zinazalishwa katika kiwanda hiki. Robot hii inakidhi mahitaji ya uhifadhi mazingira ya nchi za Ulaya, hivyo imepata orodha nyingi za uagizaji kutoka nchi hizi. Bw. Qu anasema,

    "Roboti hii ni ya kisasa duniani. Ndani ya roboti hii kuna nyaya mbili ambazo ni injini ya kuingiza umeme kwa mbali. Teknolojia muhimu ya injini hii ni kutimiza ufanisi mkubwa wa kuingiza umeme ili kuifanya roboti hii kubwa kutembea."

    Kutokana na kushikilia kufanya uvumbuzi, kampuni ya Siasun si kama tu imeyasaidia makampuni mengi ya China kuinua uwezo wa kushindana, bali pia imepata orodha nyingi za uagizaji kutoka nchi za nje. Bw. Qu Daokui anasema, sasa roboti haziagiziwi na makampuni ya kiwango cha juu tu, bali pia zinaagizwa na makampuni ya kawaida, na orodha za uagizaji zimepata ongezeko kubwa, akisema,

    "Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, orodha za uagizaji zimeongezeka kwa asilimia 108 kuliko mwaka jana wakati kama huu. Roboti zitaleta mageuzi mapya ya teknolojia na utaratibu wa uzalishaji."

    Naibu mkuu wa taasisi ya GGII Bw. Zheng Liyao anasema, mwaka huu ni mwaka muhimu kwa matumizi ya roboti nchini China. Thamani ya roboti zitakazotumiwa katika viwanda vya magari, elektroniki, vyakula na vinywaji, kemikali, plastiki na mpira, na bidhaa za metali itakuwa yuan bilioni 310 hadi 688. Uzalishaji wa roboti umekuwa injini mpya ya viwanda vya China. Bill Gates aliwahi kusema, roboti itakuwa teknolojia mpya inayobadili dunia baada ya kompyuta. Ukweli ni kwamba, roboti si kama tu itabadili njia ya uzalishaji viwandani, bali pia italeta uvumbuzi wa sayansi na teknolojia mbalimbali na maendeleo ya jamii. Kipindi kipya cha uzalishaji kinakaribia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako