Rais wa zamani wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Jacques Rogge amesema Beijing inaweza kufanya kazi nzuri kama itashinda kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mwaka 2022. Akizungumza kwenye mahojiano na shirika la habari la China Xinhua, Rogge ambaye yupo mkoani Jiangsu kwenye michezo ya pili ya Olimpiki ya Vijana, amesema China ina uwezo mkubwa wa kuandaa mashindano yoyote makubwa. Pamoja na Beijing pia kuna miji kama Oslo, Norway, na Almaty, Kazakhstan ambazo zinawania kuandaa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mwaka 2022. IOC itachagua mji wa kuandaa michezo hiyo katika kura ya siri itakayofanyika huko Kuala Lumpur Julai mwakani. Rogge ambaye aliondoka madarakani Septemba mwaka jana, ameeleza kuridhishwa na uendeshaji wa Olimpiki ya Vijana ya Nanjing na mafanikio ya michezo hiyo, iliyofunguliwa rasmi Jumamosi.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |