Makamu wa rais wa Venezuela Jorge Arreaza ameipongeza timu ya taifa ya wanariadha walioshinda medali katika michezo ya Olimpiki ya Vijana inayofanyika Nanjing, hapa China. Arreaza ametaja mafanikio ya muogeleaji Carlos Claverie na mpiganaji judo Elvismar Rodriguez kwa kupata medali za shaba katika mashindano ya kuogelea na judo. Rodriguez mwenye miaka 17, amechukua nafasi ya tatu baada ya kumshinda Mfaransa Morgane Duchene katika kitengo cha kilo 78, huku Claverie akipata shaba katika mashindano ya kuogelea mtindo wa breaststroke. Venezuela imetuma wanariadha 54 kushindana michezo 15 tofauti, katika michezo hii ya Olimpiki ya Vijana, ambayo ilianza Jumamosi na itaendelea hadi tarehe 28 mwezi huu. Mbali na hayo Arreaza pia ameipongeza timu ya mpira wa kikapu ya wanawake kwa kupata medali ya shaba katika mashindano ya mabingwa wa Amerika Kusini yanayofanyika Ecuador, baada ya kuilaza Chile kwa vikapu 72 kwa 54, na kufuzu kucheza michuano ya Pan America itakayofanyika mwakani huko Toronto Canada.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |