Libya imejiondoa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kuwania kuwa mabingwa wa Afrika mwaka 2017. Ujumbe wa taifa hilo lililogubikwa na vita umesema vita vinavyoendelea nchini humo vimewanyima fursa ya kujenga viwanja na makao ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo. Kufuatia kauli hiyo shirikisho la soka barani Afrika CAF sasa limeomba mataifa mbadala kutuma maombi ya kutaka kuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayoshirikisha timu 16. Mataifa yanayotaka kuandaa mashindano hayo yamepewa hadi septemba 30 kutuma maombi yao. Caf itatangaza mwenyeji mpya wa mashindano hayo mwakani. Shirikisho la CAF limesema linatafuta taifa lenye uwezo wa kuwahakikishia washiriki makazi, usalama, viwanja na miundo mbinu bora ya usafiri wao. Libya ilikuwa imeahidi kujenga viwanja 11 kwa gharama ya dola milioni 314 za Marekani ikiwemo uwanja wenye viti 60,000 uliokuwa unastahili kujengwa katika kambi ya zamani ya jeshi mjini Tripoli. Miji ya Benghazi na Misrata ilikuwa imeratibiwa kujengewa viwanja vipya lakini miji hiyo ndiyo iliyokuwa chimbuko la vita vilivyomng'oa madarakani Gaddafi. Tayari ligi kuu ya Libya imeahirishwa kwa hofu ya kuwa timu shiriki zitashindwa kuhakikishiwa usalama wao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |