Wanariadha wa Russia wameondoka na medali mbili za dhahabu kati ya tano zilizokuwa zikiwaniwa siku ya jumatatu kwenye mchezo wa masumbwi kwa wanaume, katika michezo ya Olimpiki ya Vijana ya Nanjing. Katika kipengele cha uzito wa kg 42 kwa wanaume, Seung Ri wa Korea Kaskazini alimshinda Faith Aslan wa Uturuki, huku kwa uzito wa kg 50, Ilkohom Bakhromov wa Uzbekistan akipata medali ya dhahabu, naye Jabbar Najafov wa Azerbajian akiondoka na fedha na Mohammadreza Aghaniachari wa Iran akinyakua shaba. Wakati huohuo Xu Shilin amekamilisha ndoto yake katika michezo hiyo katika mchezo wa tennis, kwa kumshinda Iryna Shymanovic kwa seti 6-3, 6-1 kwa upande wa wanawake na kupata medali ya dhahabu. Wakati mechi hiyo ikichelewa kwa saa zima na robo kutokana na hali mbaya ya hewa, msichana huyo mwenye miaka 16 alianza kwa kujiamni huku akizingatia kufanya vizuri kwenye mechi hiyo. Hata hivyo mechi hiyo iliwapa woga wachezaji wote wawili kwani rais wa IOC Thomas Bach, mjumbe wa IOC wa China Li Lingwei na rais wa ITF Francesco Ricci Bitti walikuwepo uwanjani wakiangalia.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |