Ethiopia na Kenya zimetangaza nia yao ya kutaka kuwania katika kinyang'anyiro cha kuwa wenyeji wa kombe la mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 baada ya Libya kujiondoa. Libya ilifikia uamuzi huo baada ya mapigano kupamba moto kati ya makundi mawili hasimu ambayo yamechelewesha mipango ya kujenga viwanja vipya vya mashindano hayo. Ethiopia, ambayo iliwahi kuwa mwenyeji wa mashindano hayo katika miaka ya 1962, 1968 na 1976, imesema itawasilisha rasmi ombi lake mara moja. Rais wa Shirikisho la soka la Ethiopia Junedin Basha amesema tayari taifa hilo lina viwanja viwili vyenye hadhi ya kimataifa, Addis Ababa na Bahir Dar, na kwamba ujenzi wa viwanja viwili vipya umefikia katika hatua nzuri. Kenya kwa upande wake imetoa taarifa ikisema nayo pia ina nia ya kuandaa mashindano hayo ikishirikiana na Tanzania, Uganda au Rwanda. Shirikisho la soka barani Afrika limetangaza tarehe 30 Septemba kuwa siku ya mwisho ya mataifa kuwasilisha maombi yao. Tangazo rasmi kuhusu nani atakayeandaa mashindano hayo litatolewa mwakani. Nalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pia limetangaza nia ya kuandaa kombe hilo. Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestin amesema wamejiridhisha kuwa wanaweza kuandaa fainali hizo kwani wana uwanja wa Taifa, pia kuna viwanja kama Arusha, Mwanza na Zanzibar, viwanja hivi vikiboreshwa na hoteli zilizopo, wanaweza kuandaa fainali hizi, amesema wameshaandaa maombi yao na watayapeleka Serikalini kwa ajili ya kupata baraka.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |