• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tunachoweza kujifunza kutoka kwa China ili tujilinde dhidi ya Ebola

    (GMT+08:00) 2014-09-01 09:23:36

    Wakati maambukizi ya Ebola unapoendelea kukithiri katika nchi tatu za Afrika magharibi, na kuingia nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya kongo hivi majuzi, wengi wetu tutakuwa tunakumbuka jinsi China ilivyosumbuliwa na homa ya mafua makali SARS, na hata changamoto nyingine za kiafya zilizotokea baada ya hapo, ikiwa ni pamoja homa ya mafua ya ndege. Wengi tulishangaa jinsi China ilivyopambana na magonjwa hayo, na kuondoa hofu ndani ya muda mfupi. Bila shaka uzoefu ilionao China katika kupambana na magonjwa ya milipuko unastahili kuigwa ili kukabiliana na hatari zinazoletwa na magonjwa ya mlipuko.

    Kwa sasa bara la Afrika na sehemu nyingine duniani ziko katika hali ya tahadhari kutokana na homa ya Ebola kutishia usalama wa maisha ya watu. Hali hiyo inalingana kiasi na hali ilivyokuwa hapa China wakati wa Homa ya SARS na inavyokuwa wakati wa mlipuko wa magonjwa mengine ya mfumo wa kupumua.

    Tofauti kubwa niliyoiona kati ya China na nchi zetu za Afrika, na inayoifanya China iwe na uhodari kwenye kupambana na magonjwa ya milipuko na ya maambukizi, ni kuwa mfumo mzuri wa kutoa taarifa za maambukizi. Bila kujali maambukizi yanatokea katika sehemu gani ya nchi, kuna idara inapewa habari kwa haraka na kupanga hatua za kushughulikia mlipuko kwa haraka. Kuna kuwa na chanzo kimoja cha kuaminika cha habari kuhusu magonjwa ya mlipuko, kwa hiyo si rahisi kuwepo kwa habari za uvumi na uzushi, kama tulivyosikia Tanzania. Baadhi ya vyombo vya habari hata vilifikia hatua ya kusema Ebola imeingia Tanzania, lakini wizara ya afya ilikanusha habari hiyo.

    Sababu nyingine ni kuwa kunakuwa na uratibu na mawasiliano mazuri kati ya idara za afya, idara za utekelezaji na usimamizi na wananchi wa kawaida. Inapotokea hali yoyote ya hatari au dharura ya afya, idara za afya zinatoa maelekezo ya namna ya kujikinga, vyombo vya habari vinafikisha haraka habari hizo kwa wananchi na kwa usahihi, na wananchi wanaitikia mwito huo bila ubishi. Kidogo hali hii ni tofauti na kwenye nchi zetu za Afrika, ambako katika baadhi ya nchi tumeona watu wanapuuza maelekezo ya idara za afya, wengine hata wanapuuza amri ya karantini ya serikali hadi kufikia hatua ya polisi na hata wanajeshi wanaagizwa kusimamia karantini.

    Kwa sasa hali ya usafiri barani Afrika inazidi kuboreka, watu wanasafiri kwa wingi kutoka sehemu moja ya nchi kwenye sehemu nyingine, au hata kutoka sehemu moja ya Afrika kwenda sehemu nyingine. Kwa China hali hii ni mara mia zaidi, kwa kuwa kila dakika watu wengi wanasafiri kwa mabasi, treni na ndege kwenda na kutoka kila pembe ya nchi, na wengine hata wanaingia kwa ndege kutoka sehemu mbalimbali duniani. Nchini China, kunapokuwa na hatari ya ugonjwa wa maambukizi, vituo vya mabasi, treni na hata viwanja vya ndege vinachukua hatua na kuwa mstari wa mbele kukagua watu wanaoingia na kutoka ili kuzuia hatari. Sehemu hizo zinawekwa wataalamu wa afya na vifaa vya kisasa kusimamia na kukagua wasafiri.

    Zaidi ya hayo, wakati wa mlipuko wa safari hii wa Ebola, China ikiwa nchi haijaathiriwa, imeshaweka mpango wa kuukinga na kuudhibiti ugonjwa huo pamona na mpango wa kuupima na utaratibu wa kuutibu ugonjwa huo. Kamati ya afya na uzazi wa mpango ya taifa imezitaka idara za afya za sehemu zote nchini kuripoti pindi wakigundua watu wanaoshukiwa kuambukizwa virusi vya Ebola au wagonjwa waliothibitishwa wa Ebola. Isitoshe, kwa wakati mmoja, wanasayansi wa China hawajajilegeza hata kidogo katika utafiti wa virusi hivyo hatari, na kufanikiwa kutengeneza kipimo cha ugonjwa huo kutokana na jeni ya virusi. Kwa sasa, kipimo hicho kimepewa idhini ya kuzalishwa na serikali, na itapunguza mchakato wa kuthibitisha wagonjwa na kuwatenga, na hivyo kuwaachia madaktari muda mrefu zaidi wa kuwatibu wagonjwa.

    China bado ni nchi inayoendelea kama nchi nyingi za Afrika, na hali yake ya kimaendeleo katika sehemu nyingi hasa vijijini na mlimani inafanana na maeneo mengi ya nchi za Afrika. Uzoefu ilioupata China wakati wa kupambana na SARS na homa ya ndege aina ya H7N9 ni kwamba lazima kuhakikisha uwazi wa taarifa kuhusu ugonjwa wa kuambukiza, na kutilia maanani kukamilisha mfumo wa afya ya umma hata wakati hamna mlipuko wa magonjwa makubwa. Nchi za Afrika zikiweza kujifunza uzoefu huo, labda tunaweza kulitaja janga hilo la Abola kama msemo wa China unavyosema: ni bahati nzuri katika wakati mbaya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako