Timu ya taifa ya Ivory Coast imesema itajitoa kwenye mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kama shirikisho la soka (CAF) litawalazimisha kucheza na Sierra Leone, Septemba 6 mwaka huu. Tembo hao wa Afrika Magharibi wamepangwa kucheza na Sierra Leone nchi iliyoshambuliwa zaidi na ugonjwa wa Ebola. Mechi hiyo ya Kundi D imepangwa kufanyika mjini Abidjan. Wakati kwa sasa kukiwa na vita vikubwa vya kupambana na virusi hivyo hatari, serikali ya Ivory Coast imetoa agizo la kutoingia nchini Sierra Leone kutokana na maradhi hayo. Rais wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast, Malick Tohe, alisema nchi yake itachukua uamuzi wa kujitoa kwenye mashindano, kama CAF itawalazimisha kucheza mechi hiyo kwa kipindi hiki ambacho kumekuwa na maradhi hayo hatari. Wakati huo huo, kocha wa Ivory Coast, Herve Renard, ameteua kikosi chake cha wachezaji 26 na kuwatema Kolo Toure na Didier Zokora. Kocha huyo ameita nyota wengine sita kwa mara ya kwanza ambao ni Ousmane Ouattara, Franck Kessie, Lamine Kone, Eric Tie Bi, Roger Assale na Gadji Tallo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |