Timu ya Kenya iliendelea kung'ara kwenye michuano ya olimpiki ya vijana ya Nanjing ya hapa China, baada ya kurejea nyumbani ikiwa na ushindi mkubwa kwa kupata jumla ya medali tano, mbili za dhahabu, mbili za fedha na moja ya shaba. Katika michezo hiyo Kenya ilikuwa ni nchi ya pili kufanya vizuri kwa timu za Afrika huku Ethiopia ikiwa ya kwanza kwa kupata medali 8, tatu za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba. Kocha mkuu wa wanariadha wa Kenya Japhet Kemei, amesema nchi yake imekosa medali zaidi katika mbio za mita 800 baada ya Agnesi Mulei na Antony Kiptoo kupata majeraha na kutolewa kwenye mashindano. Kwa sasa Kenya inalenga zaidi Olimpiki ya Rio De Janeiro mwaka 2016, ambako inatarajia kuwa wanariadha wake wachanga watashiriki michuano hiyo mikubwa na kuendelea kung'ara. Kenya imemaliza michezo ya Nanjing ikiwa nafasi ya 31 kwa ujumla, michezo ambayo imeshirikisha nchi 80. China imekuwa ya kwanza kwa kupata medali 68, 38 zikiwa za dhahabu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |