Mashindano ya mchezo wa magongo ya ligi ya dunia kwa nchi za Afrika yanaanza kesho mjini Nairobi katika uwanja wa City Park. Nchi zitakazoshiriki ni pamoja na wenyeji Kenya, Misri, Ghana na Tanzania. Nigeria ilijiondoa kutokana na ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuumiza watu vichwa. Mechi ya kwanza ya wanawake itakayofanyika kesho siku ya ufunguzi ni kati ya Ghana na Tanzania ikifuatiwa na mbili za wanaume kati ya Misri na Ghana kisha Kenya dhidi ya Tanzania. Jumamosi timu ya wanawake ya Kenya itamenyana na Ghana na baadaye mechi mbili za wanaume, ya kwanza Misri dhidi ya Tanzania na Ghana itakutana na Kenya. Jumapili mechi ya wanawake ni kati ya Tanzania na Kenya. kwa upande wa wanaume ni Ghana dhidi ya Tanzania na Kenya ikitoana jasho na Misri kwenye mechi inayotarajiwa kuwa ya kukata na shoka. Kulingana na mwenyekiti wa chama cha mchezo wa magongo cha Kenya Nashon Randiek mshindi wa mashindano ya Nairobi atafuzu kushiriki mengine kama hayo lakini na timu za hadhi ya juu nchini Afrika Kusini mwakani mwezi machi. Washindi nchini Afrika Kusini watasonga mbele na hatimaye mataifa yatakayoshinda yatafuzu kwa michezo ya Olympiki mwaka 2016 mjini Rio De Janeiro. Wakati huo huo, mwenyekiti wa chama cha kriketi cha Kenya Jackie Janmohammed amejerea tena uongozini baada ya kujiuzulu mwezi julai kwa sababu za kibinafsi. Jackie ni mwanamke wa kwanza duniani kuongoza chama cha kriketi cha taifa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |