Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amelia na safu yake ya ushambuliaji kuwa inakosa nafasi nyingi za kufunga na kuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo. Yanga iliweka kambi Pemba na Unguja na kucheza mechi tatu za kirafiki huku ikifunga mabao matano, pia ikacheza tena mchezo mwingine wa kirafiki jijini Dar es Salaam na kufunga bao moja. Yanga ilianza kwa kuifunga Chipukizi ya Pemba, kisha ikacheza na Shangani ya Unguja na kushinda kwa mabao 2-0, kabla ya kuitandika KMKM mabao 2-0. Wakati Dar es Salaam ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro. Maximo amesema anasikitishwa na hali hiyo licha ya kuwa na washambuliaji wengi kikosini, lakini wanashindwa kuzitumia nafasi wanazopata. Kocha huyo raia wa Brazil alisema mabeki wa pembeni na viungo wa timu hiyo wanatengeneza nafasi nyingi lakini washambuliaji wake wamekuwa butu, hivyo kushindwa kuipa timu hiyo ushindi mnono katika mechi zake.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |