Jinamizi la hofu limetanda Old Trafford. Hakuna anayejiamini tena katika safu yao ya ushambuliaji baada ya ujio wa nyota wa kimataifa wa Colombia, Radamel Falcao aliyekwenda kwa mkopo kutoka Monaco ya Ufaransa. Washambuliaji wawili wazoefu wa Manchester United, Robin van Persie na Wayne Rooney wanaonekana kuingiwa hofu na ujio wa Falcao na kila mtu anaonekana kuhofia nafasi yake na kwa nyakati tofauti wameahidi kuzipigania namba zao. Kwanza ameanza Van Persie kwa kupuuza madai kwamba Falcao ametua klabuni hapo kwa ajili ya kuziba nafasi yake kwa sababu anatazamiwa kufanyiwa operesheni wa goti hivi karibuni. Van Persie amekasirishwa na madai hayo. Wakati Van Persie akijitutumua, Rooney ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa nahodha mpya wa timu hiyo kuchukua kitambaa kilichokuwa kikivaliwa na Nemanja Vidic aliyetimkia Inter Milan naye alijitutumua kuhusu ujio wa Falcao. Wakati Rooney akiwa amefunga bao moja katika mechi tatu za United, Van Persie alikuwa nje baada ya kuongezewa likizo yake baadaye michuano ya Kombe la Dunia ambayo timu yake ya Uholanzi ilifika nusu fainali na alicheza kwa dakika 60 tu katika pambano dhidi ya Burnley. Falcao atavaa jezi namba 9 ya United kwa msimu mzima na anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa kudumu katika safu ya ushambuliaji Old Trafford.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |