Novak Djokovic amemshinda Andy Murray katika pambano kali la US Open na kufaulu kuingia nusu fainali. Mchezaji huyo ambaye ndie nambari moja duniani hivi sasa alishinda kwa seti tatu kwa moja ambazo ni 7-6 (7-1) 6-7 (1-7) 6-2 6-4 dhidi ya Murray katika mchuano wa saa tatu na nusu na kumalizikia saa saba na dakika 17 usiku. Katika nusu fainali Djokovic atachuana na Mjapani Kei Nishikori siku ya Ijumaa. Kushindwa kwake Murray kuna maanisha kwamba hakuweza kufaulu kucheza nusu fainali ya michuano yoyote tangu afanyiwe upasuaji wa mgongo Septemba 2013. Katika michuano ya wanawake bingwa mara tano wa US Open Serena Williams naye amefaulu kuingia nusu fainali ya michuano hiyo kwa kumshinda Mtaliano Flavia Pennettaseti kwa seti mbili ambazo ni 6-3 6-2. Ekaterina Makarova wa Urussi naye pia alifaulu kuingia nusu fainali ikiwa mara yake ya kwanza kufika hatua hiyo katika michuano mikubwa ya kimataifa. Alimshinda Victoria Azarenka kwa 6-4 6-2. Kwa upande wake mcheza Tennis wa Denmark, Caroline Wozniacki pia ametinga kwenye nusu fainali ya mashindano ya tennis kwa kumshinda mchezaji bora wa 13 duniani Sara Errani wa Italia kwa pointi, 6-0 6-1. Bingwa huyo wa zamani wa dunia sasa atacheza na Peng Shuai, wa China ambaye alifika nusu fainali yake ya kwanza ya mashindano hayo kwa kumcharaza Belinda Bencic wa Uswizi kwa seti mbili za pointi 6-2 6-1.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |