• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • AU yafanya mkutano wa dharura kuhusu mapambano dhidi ya Ebola

    (GMT+08:00) 2014-09-09 19:15:23

    Kamati ya utekelezaji ya Umoja wa Afrika jana ilifanya mkutano wa dharura kwenye makao makuu yake mjini Addis Ababa, ambapo ilitoa mwito kwa nchi wanachama wa umoja huo kushikamana na kushirikiana kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, na kuhimiza jumuiya ya kimataifa itoe uungaji mkono zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

    Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kuzifanya nchi za Afrika zichukue msimamo wa pamoja na kufuata sera mwafaka katika mapambano dhdi ya maambukizi ya Ebola. Kwenye mkutano huo mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika bibi Nkosazana Dlamini Zuma alisema mkutano huo unatakiwa kufikia makubaliano kuhusu hali ya sasa ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, na hatua za pamoja za kukabiliana na ugonjwa huo barani Afrika. Mkutano huo pia umejadili kuhusu kusitisha hatua za kupigia marufuku safari za ndege na meli kutoka nchi husika na kufunga mipaka na nchi hizo, kwa kuwa hatua hizo zimekuwa na athari mbaya kwa sifa ya nchi hizo na wananchi wao. Bibi Zuma amesisitiza kuwa hatua za pamoja zinatakiwa kuchukuliwa ili kuwasaidia watu walioathriwa na ugonjwa huo.

    Bibi Zuma ametoa mwito kwa vyombo vya habari vya Afrika, makundi yasiyo ya kiserikali, wasanii, vyama vya siasa, na mashirika mengine kushirikiana na serikali za nchi mbalimbali, mashirika ya kiuchumi ya kikanda na Umoja wa Afrika, ili kupasha habari sahihi na kwa uwazi, kuwaelimisha watu wa Afrika jinsi ugonjwa huo unavyoambukizwa, namna ya kuwatunza wagonjwa wa Ebola, na namna ya kuwazika waliokufa kwa ugonjwa huo. Pia amewataka wanasayansi wafanye juhudi kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo na kutafiti chanjo ya Ebola.

    Bibi Zuma amesema Umoja wa Afrika una wasiwasi juu ya ukarabati na maendeleo nchini Guinea, Sierra Leone, Liberia na nchi nyingine zilizoathiriwa vibaya na maambukizi ya Ebola, pamoja na athari zake kwa biashara ya kuvuka mpaka, usalama wa chakula, ajira na bei za vyakula. Amesema wakati hatua kali za kukinga ugonjwa huo zinapochukuliwa, hatua mwafaka pia zinatakiwa kuchukuliwa ili kuunga mkono maendeleo endelevu ya kilimo na biashara, na hasa kufuatilia athari za uongjwa huo kwa wanawake.

    Kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshuhulikia uchumi wa Afrika inaona kuwa, kutokana na kuwa sekta za madini, kilimo, biashara ya ndani na kimataifa, safari za ndege, uwekezaji na sekta nyingine za uchumi zote zimeathiriwa na maambukizi ya Ebola, Pato la ndani GDP katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia huenda litapungua. Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Carlos Lopes aliwahimiza watu wa Afrika wasirudi nyuma wanapokabiliana na maambukizi ya Ebola, wanatakiwa kupambana nayo kwa juhudi zote. Naibu mkurugenzi wa benki ya maendeleo ya Afrika pia amesema maambukizi hayo yakiendelea kwa muda mrefu, athari zake kwa uchumi, jamii na maisha ya watu zitakuwa kubwa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako