Uongozi wa Yanga umepanga kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kuishtaki TFF kwa kukiuka Kanuni ya 19 ya usajili katika kufanya uamuzi wa utata wa usajili wa mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi. Kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kilichofanyika jijini Dar es salaam juzi, kiliamua kumtangaza Okwi kuwa mchezaji huru baada ya kubaini kuwa Yanga ilivunja mkataba kwa kutomlipa stahiki zake za usajili na pia kuandika barua TFF kutaka mkataba wake na Mganda huyo uvunjwe, uamuzi ambao umeinufaisha Simba ambayo imemsajili. Mkataba wa mchezaji huyo ulipitiwa na kamati hiyo ikiwamo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na Yanga na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika. Kamati hiyo ilisema ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba nane kuhusu malipo ya ada ya usajili. Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho hadi kufikia Juni 27 mwaka huu, ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote. Hata hivyo, uongozi wa Yanga jUZI ulisema haukubaliani na uamuzi huo na kwamba walikuwa wameshaandika barua kupinga baadhi ya wajumbe katika kamati ya sheria ya TFF wasisikilize kesi yao, akiwamo mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya sheria. Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Katiba wa Yanga ambaye pia aliiwakilisha Yanga juzi, Sam Mapande alisema hawana imani na kamati iliyotoa uamuzi kwa kuwa kuna mgongano wa kimasilahi na TFF.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |