• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Manyonesho ya kibiashara kati ya China na Ulaya kuhimiza maendeleo ya kiuchumi mkoani Xinjiang

    (GMT+08:00) 2014-09-10 14:19:54

    Huku maonyesho ya kibiashara kati ya China na Ulaya yakiingia siku yake ya pili, majadiliano yanaendelea kuhusu mpango wa China kwa ukanda wa kisasa wa uchumi wa njia ya hariri kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Maonyesho hayo ambayo ni 4, yalifunguliwa wiki hii mjini Urumqi katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang, yalihudhuriwa na washiriki elfu 25 kutoka China na nchi nyingine 60 duniani, pamoja na wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa. Maonyesho hayo ya siku 6 yamepongezwa sana kutokana na kuchangia mafanikio ya mkoa wa Xinjiang na kuvutia uwekezaji na miradi mingi katika eneo hilo. Kwenye maonyesho ya mwaka wa 2013, zaidi ya miradi 1,000 yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 114 ilisainiwa. Kwenye maonyesho hayo, thamani ya biashara ya kigeni hivi sasa ni dola za kimarekani bilioni 5. Huku ajenda kuu mwaka huu ikiwa ni uchumi kwa kutumia njia ya Hariri, maonyesho hayo yameongeza matumaini ya kuinua maendeleo ya kiuchumi ya mkoa wa Xinjiang katika kiwango kipya. Awali, yalifahamika kama Uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mji wa Urumqi, China na nchi za kigeni, lakini sasa maonyesho hayo yamepandishwa daraja na kuwa ya kimataifa tokea mwaka wa 2011. Mabadiliko hayo yameongeza umaarufu wa maonyesho hayo ambapo wafanya biashara wengi kutoka nchi za nje wamekuwa wakisafiri katika eneo hilo kutafuta nafasi za kibiashara. Kwa mujibu wa waandaaji wa maonyesho hayo, zaidi ya nchi 30 zilishiriki kwenye maonyesho ya kwanza ya CEE, huku thamani ya biashara ya nje ikiwa ni dola za kimarekani bilioni 5.51. Maonyesho hayo yameendelea kupata umaarufu kote duniani. Mwaka wa 2013, CEE ilikaribisha mashirika saba ya kimataifa pamoja na nchi mbalimbali kuhudhuria maonyesho hayo ya tatu. Mkuu wa maonyesho ya kimataifa ya Xinjiang Bw Li Jingyuan anasema, lengo lao ni kuzileta pamoja nchi jirani kujadili mikakati ya maendeleo. Katika maonyesho ya mwaka huu, vikao mbalimbali vimeandaliwa ili kuongeza mawasiliano ya kisiasa, uchumi ,biashara na nishati. Amesema vikao vya kujadilia ukanda wa uchumi wa njia ya Hariri, ubunifu wa kiufundi pamoja na mfumo wa satelaiti wa Beidou vitasaidia kuhimiza mawasiliano ya kiuchumi na kuvutia wawekezaji wengi mkoani Xinjiang. Amesema majadiliano kuhusu sekta ya matunda ya Xinjiang yatakuwa yenye manufaa makubwa kwa kuwa eneo hilo linajivunia jiografia ya kipekee. Bw Li ameongeza kuwa, wataalam kutoka China, Russia na Kazakhstan, pamoja na wengine wengi watabadilishana mawazo kuhusu kilimo pamoja na soko la matunda na hata kusaini mikataba itakayotoa nafasi nzuri kwa matunda ya Xinjiang kupenya katika soko la kimataifa. Anaongeza kuwa, nafasi kwa wawekezaji ama wale wanaotaka kuwekeza ni kubwa. Katika maonyesho ya mwaka jana, kampuni ya ujenzi na uzalishaji ya Xinjiang ilifanikiwa kuanzisha miradi kadha yenye thamani ya yuan bilioni 221 katika eneo hilo. Naye mkuu wa kampuni ya Tianhonglihao Investment Bw Pan Li aliwekeza jumla ya yuan bilioni 10 katika mradi wa ujenzi katika mji wa Wujiaqu mwaka jana. Mradi huo unajivunia rasilmali za utalii, biashara, maeneo ya makazi pamoja na sehemu za burudani. Bw Pan anasema, jambo lililomfanya awekeze Xinjiang ni kutokana na mustakabali mzuri wa eneo hilo.

    Katika ufunguzi wa maonyesho hayo, naibu waziri mkuu wa China Bw Wang Yang aliahidi kuunga mkono ujenzi wa ukanda wa kiuchumi wa njia ya Hariri ambao ulipendekezwa na rais Xi Jinping wakati wa ziara yake katika Asia ya kati Septemba mwaka jana. Ukanda huo unalenga kufufua utamaduni wa njia hiyo ambayo kihistoria iliunganisha China na Asia ya kati pamoja na Ulaya, kwa kujenga uhusiano wa kisiasa na kiuchumi. Kufufuliwa kwa mradi huo kunahusisha zaidi ya nchi 40 kutoka Asia na Ulaya ambazo kwa pamoja zina jumla ya watu bilioni 3. Mkoa wa Xinjiang unaiunganisha China na nchi za Mongolia, Pakistan, Russia, India pamoja na nchi nyingine za Asia ya kati ambapo ni rahisi kufikia soko la Ulaya. Urumqi ndio sehemu ambayo njia ya hariri ilipitia. Xinjiang hivi sasa haitaki kuachwa nyuma na inalenga kujijenga na kuwa kituo muhimu cha usafiri, biashara, fedha, utamaduni na huduma za afya kwenye ukanda huo. Mtafiti wa masuala ya kiuchumi Bw Wang Ning anasema, maonyesho ya CCE yataendelea kuwa kiungo muhimu cha uchumi wa Xinjiang, haswa wakati huu ambapo mkoa huo unaendelea kuwa na ushawishi mkubwa kwenye ukanda wa kuchumi wa njia ya Hariri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako