Ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga imeendelea kwa michezo kadhaa kuchabangwa ambapo FC Barcelona waliikaribisha Athletic Bilbao kwenye dimba la Nou Camp. Mchezo huo ulimalizika kwa matokeo ya ushindi wa 2-0 kwa FC Barcelona. Akiwa anahitaji magoli mawili tu kufikisha jumla ya magoli 400 katika maisha yake ya soka, Lionel Messi alishindwa kutimiza idadi hiyo lakini badala yake aliweza kusaidia mara mbili kupata magoli ya ushindi ambayo yote yalifungwa na Neymar. Wakati huohuo mabao mawili ya Thiago na Arda Turan wa Atletico Madrid yamezidi kuipa mwanzo mbaya klabu ya Real Madrid kwenye michuano ya kugombea ubingwa wa La Liga baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-1 kwenye mchezo wa 'Madrid Derby' uliopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu. Cristiano Ronaldo alifunga goli la kufutia machozi la Real Madrid lakini halikutosha kuwapa matokeo mazuri vijana wa Carlo Ancelloti. Hiki ni kipigo cha pili kwa Madrid katika kipindi cha siku 14, wiki mbili zilizopita walifungwa 4-2 na Real Sociedad.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |