Ligi ya mabingwa wa ulaya imeendelea tena jana kwa michezo kadhaa kupigwa katika viwanja mbalimbali barani ulaya, kule Etihad stadium Manchester City waliikaribisha FC Bayern Munich katika mchezo wa kundi E. Mchezo huo uliowakutanisha mabingwa wa ligi za Ujerumani na England ulikuwa mgumu na mpaka kufikia dakika ya 90 bado matokeo yalikuwa 0-0, sifa zimuendee Joe Hart wa City kwa umahiri wa kuokoa michongo ya washambuliaji wa Bayern. Katika dakika 3 za mwisho za nyongeza mchezaji wa zamani wa Man City, Jerome Boateng akaiadhibu timu yake ya zamani kwa kuifungia Bayern goli pekee na la ushindi kwenye mchezo huo. Boateng alifumua shuti kali ambalo Hart alijaribu kulifuata lakini likamshinda na kuipa Bayern ushindi wa kwanza. Wakati huohuo baada ya msimu uliopita kuishia kwenye hatua ya nusu fainali, klabu ya Chelsea jana ilianza upya mbio zake za kuutaka ubingwa wa Champions League kwa kucheza dhidi ya Schalke. Huku ikimuanzisha Didier Drogba badala ya Diego Costa, Chelsea wameambulia sare ya 1-1 dhidi ya Schalke ya Ujerumani. Cesc Fabregas alianza kuifungia Chelsea goli katika kipindi cha kwanza kabla ya Klaas Jan Huntelaar kuisawazishia Schalke muda mfupi tu baada kipindi cha pili kuanza.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |