Polisi ya Merseyside imesema inachunguza ujumbe wa ubaguzi wa rangi aliotumiwa mshambuliaji wa Liverpool Mario Baloteli kupitia Twita. Muitaliana huyo alipokea ujumbe wa ubaguzi wa rangi baada ya kutweet "Man United….LOL" baada ya United kukandamizwa bila huruma magoli 5-3 jana Jumapili. Ujumbe wa mchezaji huyo mwenye miaka 24, ulijibiwa kwa zaidi ya mara laki 1 na nusu na ndani kukiwa na mlolongo mkubwa wa ujumbe wa ubaguzi wa rangi. Tokea hapo anuani nyingi zilizotumika kutuma ujumbe huo zimefungwa. Polisi imesema kwanza wanataka kujua nani aliyetuma ujumbe huo na unatokea wapi. Nalo kundi linalopinga ubaguzi wa rangi, limesema watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wametahadharishwa kuhusu tweet hizo za kibaguzi alizotumiwa mchezahi huyo wa zamani wa Manchester City. Pia msemaji wa kundi hilo amesema kundi linamuunga mkono Mario Balotelli kwa yote yaliyomkumba. Katika kipindi kirefu cha nyuma Balotelli amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo na watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wa kikosi cha Italia wakati wa mazoezi kabla ya kombe la dunia, wakati alipokuwa Inter Milan na hivi karibuni AC Milan.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |