Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal anasema anamshangaa Pep Guardiola kwa kusema mengi kuhusu mastaa wake wa Bayern Munich wakati wote wanapenda kutua Old Trafford. Guardiola alimpiga kijembe Van Gaal wiki iliyopita kwamba Man United haina pesa za kuwanunua mastaa wake kama Arjen Robben, Bastian Schweinsteiger na Thomas Muller, ambao kwenye kipindi cha majira ya joto walihusishwa na timu hiyo ya Ligi Kuu England kabla ya kuamua kubaki Allianz Arena. Lakini, Van Gaal alisema anashangaa Guardiola amepata wapi ujasiri huo wakati wakali hao wote aliowataja wanataka kuichezea United. Van Gaal alisema: "Sina haja ya kuzungumza alichosema. Nadhani kila mchezaji ambaye nilifanya naye mawasiliano anataka kuichezea Manchester United.
"Utashangaa licha kwamba hatupo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wachezaji wanataka kuja kucheza hapa. Hiyo inashangaza, lakini ni kutokana na ukubwa wa klabu na mipango thabiti iliyoanzishwa kwa sasa." Robben alihusishwa na mpango wa kujiunga na United kabla ya timu hiyo kumsajili Angel di Maria. Van Gaal pia alikaribia kuwanasa Muller na Holger Badstuber, ambao wote walianza kuichezea Bayern wakati alipokuwa kocha wa timu hiyo ya Allianz Arena. Mdachi huyo alisema hakuwa na mpango wowote wa kumsajili mchezaji yeyote wa Bayern na kama mchezaji wa timu hiyo angependa kutua Old Trafford hilo lingetokea kama tu Bayern wangekubali. Alipoulizwa kuhusu kauli ya Guardiola kama ilikuwa na ukweli kwamba United iliwataka wachezaji wa Bayern, Van Gaal alisema: "Watu wanadhani kwamba kila kinachoandikwa kwenye vyombo vya habari ni sahihi. Lakini, wakati mwingine si kweli."
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |