Kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani FIFA vilivyotangazwa Alhamis, timu ya taifa ya Uganda imepanda nafasi mbili juu ambapo sasa ipo nafasi ya 79. Uganda pia imepanda hadi nafasi ya 19 katika bara la Afrika. Baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Ghana, ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Guinea katika michuano ya kufuzu kucheza kombe la mataifa ya Afrika mwakani, Uganda sasa imejikusanyia pointi 418 na kuwa juu ya Australia, Trinidad na Tobago na Morocco miongoni mwa nyingine. Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uganda Milutin 'Micho' Sredojevic amesema anafuraha kuona timu yake inajitahidi na kiwango chao kinaboreka. Algeria ambayo ipo nafasi za juu kwa nchi za Afrika pia imepanda nafasi nne juu na kukamata nafasi ya 20 duniani, huku Cote d'lvoire ikiwa ya pili kwa kukamata nafasi ya 22. Misri ambayo kwa sasa haipo katika hali nzuri imeshuka kwa nafasi 23 na kukamata nafasi ya 61. Mabingwa wa zamani wa Afrika Zambia pia nao wameporomoka hadi nafasi ya 88.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |