Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema litakula jino kwa jino na wahalifu waliojiingiza kutengeneza tiketi feki za elektroniki na kueleza kuwa tayari wametoa taarifa hizo kwa Jeshi la Polisi ili liweze kufuatilia uhalifu huo. Kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa wikiendi iliyopita kulishuhudiwa wingi wa tiketi feki zilizokamatwa na maofisa wa TFF baada ya kushindwa kutambuliwa na mashine za ukaguzi hasa katika mechi ya Mtibwa na Yanga mjini Morogoro. Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Boniface Wambura alisema TFF haitafumbia macho vitendo hivyo lakini pia amewataka wananchi kuwa waangalifu wanapofanya manunuzi ya tiketi hizo kwa kutumia njia zilizowekwa na si kununua mitaani. Mbali na sakata la tiketi feki, Wambura alisema kwenye mechi ya Mtibwa na Yanga, idadi ya watu waliojitokeza ilikuwa kubwa kuliko idadi ya tiketi, walikwishauza tiketi 11,599 ambazo zilikwisha mapema na hiyo ndiyo ilikuwa idadi ya mwisho kutokana na uwezo wa Uwanja wa Jamhuri.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |