Nahodha wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan, amekanusha madai kuwa alimtoa kafara rafiki yake ambaye pia alikuwa mwanamuziki mashuhuri nchini Ghana Castro. Gyan amesema tetesi hizo ni za kushangaza sana wala hazina msingi. Mwanamuziki huyo aliyekuwa anaiimba nyimbo za mtindo wa Afrobeats, ambaye jina lake halisi ni Theophilus Tagoe, alitoweka pamoja na rafiki yake Janet Bandu, mnamo mwezi Julai wakati walipokwenda likizo na Gyan ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Sunderland, katika mji wa Ada. Madai katika vyombo vya habari nchini Ghana yanasema kuwa kutoweka kwa rafiki ya Gyan kumezua wasiwasi huku wengine wakidai kuwa huenda alimtoa kafara mwanamuziki huyo. Castro na rafiki yake Bandu, walionekana mara ya mwisho wakielekea baharini na baadaye iliarifiwa kuwa walizama. Miili ya wawili hao haikuwahi kupatikana na madai yaliendelea kusambazwa mwezi huu wakati ambapo kakake Gyan, Baffour Gyan alidaiwa kuwa mmoja wa genge la vijana waliowashambulia waandishi wa habari waliohoji maswali kuhusu madai hayo. Hata hivyo baadaye aliachiliwa na polisi waliokuwa wamemkata kwa lengo la kumfungulia mashitaka. Tetesi hizo zilimfanya Gyan kuitisha mkutano na wandishi wa habari kuzungumzia madai hayo. Wakili wake Kissi Agbyabeng alitoa taarifa akisema kuwa familia ya Gyan imeshangazwa sana na madai hayo na iliamua kutosema chochote ili polisi waendelee na uchunguzi wao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |