Mwanariadha wa Kenya Dennis Kimetto amevunja rekodi ya dunia katika mbio za Marathon zilizoandaliwa mapema jana mjini Berlin nchini Ujerumani. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 30 alishinda mbio hizo kwa muda wa saa mbili, dakika mbili na sekunde 57 ambapo aliivunja rekodi ya awali kwa sekunde sita. Rekodi ya awali iliwekwa na mkenya mwenzake Wilson Kipsang katika mbio hizo mwaka uliopita. Bingwa huyo aliwashinda maelfu ya wakimbiaji walioshiriki mashindano hayo. Kimetto ameonesha kuwa hashindikani katika mbio hizo ndefu kwa kushinda Tokyo na Boston mwaka jana. Aliahidi kuvunja rikodi katika mbio za Berlin kama hali itaruhusu ambapo alitimiza ndoto yake hiyo. Kwa upande wa wanawake Tirfi Tsegaye alishinda mbio hizo kwa kutumia muda wa saa 2:20:18, sekunde 8 tu mbele ya muethiopia mwenzake Feyse Tadese ambaye alikuwa wa pili huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Mmarekani Shalane Flanagan.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |