Hatimaye staa wa Manchester United na nahodha wa timu hiyo, Wayne Rooney ameomba samahani kwa kusema alichemsha baada ya kupewa kadi nyekundu ya kijinga katika pambano dhidi ya West Ham Jumamosi. Rooney, ambaye ni maarufu kwa jina la Wazza alipewa kadi hiyo katika dakika ya 60 ya mchezo Old Trafford baada ya kumrukia kwa nyuma winga wa West Ham, Stewart Downing huku akimpa kazi rahisi mwamuzi Lee Mason kumpa kadi nyekundu. Man United ilifanikiwa kuzoa pointi zote tatu kwa ushindi wa mabao 2-1 licha ya Rooney kuwa nje, lakini hatimaye Rooney amewaomba radhi wachezaji wenzake huku akifafanua kosa lake. Kuongeza chumvi katika kidonda, kocha wa Manchester United Louis van Gaal pia alikiri kwamba kadi nyekundu aliyopewa Rooney ilikuwa halali na hana malalamiko nayo. Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Dwight Yorke amedai kwamba hawezi kumsamehe Rooney kwa kitu alichofanya. Kwa kuonyeshwa kadi hiyo nyekundu, Rooney atalikosa pambano la Jumapili ijayo dhidi ya klabu yake ya zamani, Everton huku pia akilikosa pambano dhidi ya West Brom Jumatatu ya Oktoba 20. Pigo kubwa zaidi kwa Manchester United litakuja mwishoni mwa mwezi ujao wakati Rooney atakapolikosa pambano dhidi ya Chelsea katika Uwanjani la Old Trafford.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |