Usiku wa juzi watu wawili waliowahi kuwa vipenzi vya nchi ya Ureno Jose Mourinho na Nemanja Matic walirejea tena nchini humo katika jiji la Lisbon lakini safari hii wakiwa kama wapinzani. Wakati Mourinho akionekana kuwa kivutio kikubwa kwa vyombo vya habari ndani ya jiji la Lisbon, Nemanja Matic alikuwa kasahaulika kabisa. Lakini katika dakika ya 34, mchezaji huyo wa zamani wa Benfica aliifungia goli pekee Chelsea katika mchezo huo. Matic alifunga goli hilo kwa kichwa baada ya kuachwa bila kukabwa vizuri na mabeki wa Sporting Lisbon. Mchezaji wa zamani wa Manchester United Luis Nani alikuwa akiitumikia Sporting na hakuwa kwenye kiwango kizuri katika kipindi cha kwanza, kipindi cha pili alijitahidi lakini akashindwa kubadili matokeo ya mwisho dhidi ya vijana wa Jose Mourinho.
Nao Mabingwa wa ligi kuu ya Uingereza klabu ya Manchester City imeendelea kutopata matokeo mazuri katika michuano ya ligi ya mabingwa wa ulaya kwa mara ya pili mfululizo msimu huu. Wakicheza kwenye uwanja wao wa Etihad dhidi ya AS Roma ya Serie A, Sergio Aguero aliipatia timu yake goli katika dakika ya 4 kupitia mkwaju wa penati. Lakini dakika 19 baadae Francisco Totti 'Mfalme wa Roma' akaifungia goli la kusawazisha Roma na kuandika historia ya mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga goli kwenye michuano ya ulaya. Man City sasa inakuwa imeshindwa kupata matokeo chanya katika mechi 2 za kwanza za kombe la mklabu bingwa za Ulaya. Wiki mbili zilizopita walifungwa na Bayern Munich.
Naye mwanasoka wa kibrazil David Luiz juzi usiku alikuwa mchezaji wa kwanza kuifunga goli FC Barcelona katika msimu mpya wa soka barani ulaya. Luiz alifunga goli hilo katika dakika ya 11 ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa kati ya klabu PSG dhidi ya Barca. Mchezo uliopigwa kwenye dimba la Stade de France na kuhudhuriwa na mastaa kama Rais wa zamani wa nchi hiyo Sarkozy, David Beckham na rapa Jay Z pamoja na mkewe Beyonce. Matokeo ya mchezo huo ni ushindi wa 3-2 kwa PSG dhidi ya kikosi cha Luis Enrique. Lionel Messi na Neymar walifunga magoli ya Barca huku Matuidi na Verrati wakihitimisha kipigo hicho cha kwanza cha Barcelona katika michuano yote ya msimu huu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |