Patrick Kluivert yupo kwenye orodha ya watu watano ya shirikisho la soka la Ghana ambao wanawania kuwa kocha wa timu hiyo. Ghana imekuwa haina kocha tangu Kwesi Appiah aondoke mwezi septemba. Wagombea wengine ni pamoja na bosi wa zamani wa Chelsea Avram Grant, kiungo wa kati wa zamani wa Italia Marco Tardelli, Mswissi Michel Pont na Mhispania Juan Ignacio Jimenez. Kluivert mwenye miaka 38 ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Ajax na Barcelona aliyefunga magoli 40 katika mechi 79, ameondoka kwenye nafasi yake ya msaidizi kocha wa timu ya Uholanzi baada ya kombe la dunia. Kluivert ameanza kazi ya ukocha mwaka 2011 ambapo aliishughulikia timu ya vijana na timu ya akiba. Mwaka mmoja baadaye akawa msaidizi wa kocha wa Uholanzi Louis van Gaal na wawili hao wakaifikisha timu yao hadi nafasi ya tatu katika kombe la dunia la Brazil. Black Stars hivi sasa wanasimamiwa na Maxwell Konadu na ataiongoza timu hiyo katika mechi ya kufuzu kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2015 dhidi ya Guinea ambapo wanatarajiwa kucheza Oktoba 11 huko Morocco kabla ya kucheza mechi ya marudiano siku nne baadaye nchini Ghana. Wakati huohuo mfaransa Corentin Martins ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Mauritania. Kocha huyo mwenye miaka 45 anachukua nafasi ya Patrice Neveu ambaye alifukuzwa mwezi Agosti baada ya timu hiyo kutolewa kwenye michuano ya kufuzu kucheza kombe la mataifa ya Afrika mwakani. Martins amewashinda wafaransa wenziwe Pierre Lechantre na Sebastien Desabre na Mserbia Milovan Rajevac.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |