Kampeni za kutafuta tiketi ya kufuzu kuelekea nchini Ufaransa mwaka 2016 kwenye michuano ya soka ya mataifa bara la Ulaya ziliendelea tena usiku wa kuamkia jana wakati timu kadhaa ziliposhuka dimbani. Mabingwa watetezi Hispania walikuwa wageni wa Luxembourg, hadi mwisho wa mchezo huo wageni Hispania wakafanikiwa kuibuka washindi baada ya kuwaadhibu wenyeji wao kwa jumla ya mabao 4-0. Nayo Russia ilishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kukubali kugawana pointi na wageni wao Moldova kwa kutoka sare ya bao 1-1. Kwingineko England iliibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Estonia. Nako Sweden kukawa na hekaheka zilizowakutanisha wenyeji Sweden dhidi ya Liechtenstein. Hadi mwisho wa mchezo huo wenyeji wakafanikiwa kuwagaragaza wapinzani wao kwa jumla ya mabao 2-0. Austria ikaisambaratisha Montenegro kwa jumla ya goli 1 kwa bila, wakati Slovenia walipowavunjia heshima wenyeji wao Lithuania kwa kuwasasambua bila huruma kwa mabao 2-0 huku Belarus ikitafuta majibu ya kuwapa mashabiki wake baada ya kudondokea pua kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Slovakia.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |