Arsene Wenger ameomba radhi kwa kitendo chake cha kumkunja shati na kumsukuma kocha mwenzake, Jose Mourinho Jumapili iliyopita, lakini Mfaransa huyo amedai alichokozwa. Wenger alimfuata Mourinho na kushikana naye wakati Arsenal ilipomenyana na Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu England Uwanjani Stamford Bridge na wenyeji kushinda mabao 2-0. Makocha hao walijikuta wakishikana baada ya Wenger kukerwa na beki wa Chelsea, Gary Cahill alipomchezea rafu mshambuliaji wake, Alexis Sanchez. Wenger alisema wamelipa umuhimu mkubwa sana jambo hilo na kwamba hakuingia kwenye eneo la benchi la Chelsea. Ameomba radhi kwa kusema asingepaswa kuhamaki vile, na anajuta kwa kila kitu. Hata hivyo alisisitiza kuwa Mourinho alimchokoza na huo ndio ukweli. Wenger, 64, amekuwa na upinzani na Mourinho kwa miaka mingi sasa tangu Mreno huyo alipowasili kwenye Ligi Kuu England mwaka 2004 na hivi karibuni alimwita kuwa ni bingwa wa kufeli.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |