Mwandishi Marti Perarnau ambaye alizunguka mwaka mzima na kocha kijana Pep Guardiola kwa ajili ya kuandika kitabu cha msimu wake wa kwanza akiwa na Bayern Munich amefichua kwamba kocha huyo anatazamia kuwa kazi yake inayofuata itakuwa England. Kauli hiyo huenda ikazua vita kwa klabu mbalimbali kubwa za England ambazo zitapenda huduma yake. Kwa sasa Guardiola ana mkataba na Bayern Munich mpaka mwaka 2016 akiwa anatokea Barcelona ambapo alijijengea jina kubwa kwa kutwaa mataji mawili ya ubingwa wa Ulaya, mataji matatu ya La Liga, mawili ya Kombe la Mfalme, mawili ya Super Cup, na mawili ya Klabu Bingwa ya Dunia. Manchester City inapewa nafasi kubwa ya kumchukua Guardiola kutokana na urafiki wake mkubwa na mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, Txiki Begiristain, ambaye alicheza naye Barcelona na pia aliwahi kushika nafasi hiyo ya ukurugenzi wa ufundi Barcelona wakati Guardiola akiwa kocha. Hata hivyo, kwa uamuzi wake wa kutaka kwenda England utaiweka Arsenal katika tahadhari wakati huu bosi mtendaji wa timu hiyo, Ivan Gatzidis akikiri kwamba kunahitajika umakini mkubwa kumpata kocha mbadala kuchukua nafasi ya Arsene Wenger mwenye umri wa miaka 65.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |