Kocha Carlo Ancelotti amefuta kabisa ndoto za Cristiano Ronaldo kurudi Manchester United baada ya kufichua kwamba staa huyo Mreno atazeekea Real Madrid. Ronaldo ameonyesha kuwa mwanasoka bora kabisa duniani kwa sasa katika kipindi cha miaka yake mitano klabuni Real Madrid tangu alipojiunga na timu hiyo kwa ada ya uhamisho wa Pauni 80 milioni akitokea Man United mwaka 2009. Mwaka huu kumekuwa na uvumi kwamba huenda Mreno huyo akarudi Old Trafford mwakani, lakini Ancelotti ameibuka na kudai kwamba Real Madrid inamhitaji mwanasoka huyo bora kubaki kwenye kikosi chao. Kocha huyo amesema kila mtu anaweza kubadilishwa au kutolewa, lakini Ronaldo kwa sasa ni mwanasoka bora duniani na kumpoteza hilo litakuwa pigo kubwa kwa Real Madrid. Ancelotti pia amesisitiza kuwa hilo haliwezi kutokea, Ronaldo ataendelea kubaki Real Madrid kwa kipindi chote cha maisha yake kwenye mchezo huu. Amewahakikishia mashabiki wa Real kwa asilimia 100 kwamba Ronaldo atabaki Madrid msimu ujao na si kwenda Manchester United, kwani amesema mchezaji huyo anafurahia kuwa Real na anapendwa na kila mtu hivyo atamaliza maisha yake ya soka akiwa Real.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |