Klabu ya Liverpool imepewa somo la kuumiza moyo juu ya ligi ya mabingwa wa Ulaya jinsi iliyobadilika, baada ya kugaragazwa kwa mabao matatu bila jawabu na Real Madrid katika uwanja wa Anfield. Christiano Ronaldo alikuwa wa kwanza kufungua ukurasa katika dakika ya 23 na bila kutoa hata nafasi ya kupumua dakika mbili tu baadaye Benzema akaongeza la pili na kuwafanya Liverpool waanze kugwaya wasijue la kufanya. Kabla hata mapumziko katika dakika ya 41 Benzema huyohuyo akashindilia msumari wa moto kwenye kidonda kwa kuongeza bao la tatu na kuwafanya Real waondoke kifua mbele. Nayo Chelsea kwa upande wake ilitoa kipigo kizito zaidi katika ligi ya mabingwa wa Ulaya baada ya kuiadhibu klabu ya Maribor kwa magoli 6 kwa nunge. Magoli ya Chelsea yalifungwa na Remy, Drogba, Terry, Viller na Hazard. Kama hayo hayatoshi klabu ya Bayern Munich iliamua kuwakumbusha mashabiki wa AS Roma kipigo cha mabao 7-1 walichokipata kutoka kwa Manchester United mwaka 2007-08, katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Stadio Olimpico jijini Rome, Italia. Bayern waliipa AS Roma kipigo hicho kupitia magoli ya Arjen Robben aliyefunga magoli 2, Lewandoski, GOtze, Riberry, Muller, na Shaqiri. Mbali na mvua hiyo ya magoli, FC Barcelona pia ikaichakaza Ajax FC ya Uholanzi kwa kipigo cha magoli 3-1. Lionel Messi alimfikia Cristiano Ronaldo kwa jumla ya magoli kwenye michuano ya Ulaya, baada ya kufunga goli ambalo limemfanya atimize magoli 69. Naye Neymar alifunga la 2 na Sandro Ramirez akamalizia kwa kufunga la 3.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |