Ndoa ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF na Kampuni ya Bia Tanzania TBL sasa iko mashakani baada ya kampuni hiyo kubwa nchini Tanzania kutishia kusitisha udhamini wake wa zaidi ya Shilingi bilioni 17 kutokana na kubaini matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha. TBL na TFF zilisaini mkataba huo wa udhamini wa timu ya Taifa ya soka, Taifa Stars mwaka 2012 ukiwa na thamani ya Dola milioni 10 za Marekani kwa miaka mitano na huu ni mwaka wa pili wa mkataba huo wa kihistoria kwa ukubwa ambao ulianza Mei, 2012. Habari zinasema, ufisadi huo uligundulika kwenye akaunti ya fedha za udhamini wakati wa ukaguzi wa robo nne za mwisho katika kipindi cha udhamini kinachoishia Mei, 2014. Ukaguzi huo ulionyesha kuwa kulikuwa na matumizi ya zaidi ya Dola 903,000 (sawa na zaidi ya Sh1.4 bilioni) ambayo yalifanywa bila ya kuheshimu masharti ya mkataba na kwa kukiuka kanuni za fedha za TFF. Hata hivyo, mkurugenzi wa masoko wa TBL George Kavishe, alimwandikia Rais wa TFF Jamal Malinzi kueleza kusikitishwa na kitendo cha shirikisho hilo kushindwa kuonyesha vielelezo vya kuthibitisha matumizi hayo, licha ya wakaguzi kuwapa fursa ya kujibu na kuwasilisha vielelezo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |