Serena Williams juzi aliendeleza makeke yake na kufanikiwa kumshinda Simona Halep, ushindi ambao ulimpatia taji la fainali za kumalizia msimu za WTA kwa miaka mitatu mfululizo katika michuano iliyofanyika Singapore. Serena alishinda kwa pointi 6-3 6-0 na kupata taji hilo kwa mara ya tano sasa. Serena pia alilipiza kisasi cha kubamizwa vibaya katika kipindi cha miaka 16 dhidi ya Halep katika hatua ya makundi. Mchezaji huyo mwenye miaka 33, ambaye alishinda michuano ya 18 ya Grand Slam katika mashindano ya US Open mwezi Septemba, anamaliza mwaka akiwa namba moja duniani kwa mara ya nne. Na kwa upande wa michuano ya Valencia Open mcheza tenisi wa Scotland Andy Murray akaonesha ubabe wake dhidi ya Muhispania Tommy Robredo na kufanikiwa kushinda taji hilo. Murray ambaye pia alimshinda Robredo kwenye michuano ya Shenzhen mwezi uliopita, alishinda kwa pointi 3-6, 7-6 (9-7) 7-6 (10-8), baada ya kupambana kwa saa 3 na dakika 20.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |