Nigeria inakabiliwa na marufuku ya kushirikishi shughuli zozote zinazohusiana na soka kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA, hatua ambayo kama itafikiwa, itaifanya nchi hiyo ikose kushiriki mashindano yajayo ya kombe la mataifa ya Afrika. Marufuku hiyo inafuatia uamuzi wa mahakama kuu ya Jos, juu ya uchaguzi wa hivi karibuni wa shirikisho la Soka la Nigeria NFF. Mahakama hiyo ilibatilisha uchaguzi uliofanyika septemba 30 ambao ulishuhudia Amaju Pinnick akiibuka kuwa rais wa shirikisho hilo. Nigeria imeshapigwa marufuku mara mbili kwa kitendo cha serikali yake kuingilia NFF, na Fifa iliionya kuwa nchi hiyo ikifanya tena itafungiwa hadi Mei mwaka 2015. Kombe la mataifa ya Afrika limepangwa kufanyika kuanzia Januari 17 hadi Februari 8. Hii inamaanisha kuwa Nigeria wakifuzu kucheza michuano hiyo, watapoteza nafasi yao kama Fifa ikichukua hatua juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama. Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika Issa Hayatou jumamosi alikutana na maofisa wa Nigeria huko Windhoek, Namibia kwenye fainali za wanawake za mabingwa wa Afrika ambapo Super Falcons iliishinda Cameroon. Vyombo vya habari vya nchi hiyo vikaripoti kuwa Hayatou amemuambia waziri wa michezo Tammy Danagogo kwamba kama amri ya mahakama haijatenguliwa, Fifa itabidi iipige marufuku nchi hiyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |