Winga ghali nchini Uingereza, Angel Di Maria, amesema anamshangaa kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, anayesema kwamba ameondoka kwenye timu hiyo kwa sababu ya tamaa ya pesa. Staa huyo Muargentina anayelipwa Pauni 200,000 kwa wiki klabuni Manchester United baada ya kujiunga kwa ada ya Pauni milioni 60, alisema pesa si kitu kilichomfanya ahame Real Madrid bali ni mapenzi ya kwenda kuichezea timu hiyo ya Old Trafford. Di Maria anasema amekuwa na hisia kali kwa uhamisho wake huo wa Man United na kusisitiza kuwa anajivunia kwa jambo hilo kutokea. Amesema alitaka mwenyewe kwenda kucheza United kwani alitaka kuvaa jezi za timu hii. Di Maria ameongeza kuwa ni jambo zuri kwake kuvaa namba 7, kwasababu ilivaliwa na wachezaji magwiji na yeye anataka kuwa mmoja wao. Pia alisema anadhani watu wa huko wanamfurahia, hivyo ni lazima aiheshimu jezi hiyo. Di Maria ameanza vizuri kwenye kikosi hicho cha Man United licha ya kwamba timu hiyo bado inasuasua kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |