Uamuzi juu ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika kama zitaendelea kuchezwa Januari au zitaahirishwa kwa sababu ya hofu ya virusi vya Ebola unatarajiwa kutolewa leo baada ya serikali ya Morocco kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka la Afrika. Mkutano huo utakaofanyika Rabat ulipangwa mwezi uliopita kufuatia Morocco kuiandikia Caf na kuiomba kuahirisha mashindano hayo, baada ya kushauriwa na wizara yake ya afya kwamba kukaribisha timu 16 nchini humo kutasababisha hatari kubwa ya kuenea kwa virusi hivyo hatari. Hata hivyo Caf ilikataa mara moja na kusisitiza kuwa shindano la wiki tatu litaendelea kama lilivyopangwa kuanzia Januari 17 hadi Februari 8. Na kuanzia hapo Caf imeziomba takriban nchi 7 kama zinaweza kuwa wenyeji wa michuano lakini haijapata jibu zuri. Mkutano uliofanyika jana wa kamati tendaji ya Caf huko Algiers ulikuwa ni wa kuamua msimamo wa Caf kwenye mazungumzo ya leo na maofisa wamesema taarifa ya matokeo itatolewa mapema leo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |