Kilabu ya Entente Satif kutoka Algeria imechukua taji la klabu bora barani Afrika kwa mara ya kwanza katika miaka 26 baada ya kuishinda klabu ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mabao ya ugenini kufuatia sare ya 3-3 siku ya jumamosi. Raundi ya pili ya fainali katika uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida iliisha kwa sare ya 1-1, siku sita tu baada ya sare ya 2-2 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa mjini Kinshasa. Setif ndio iliyoanza kuona lango la wapinzani wao kupitia Sofaine Younes ambaye alifunga bao kupitia pasi ya El Hadi Belameiri dakika nne baada ya kuanza kipindi cha pili. Lakini wageni hao walisawazisha dakika tano baadaye kupitia Lema Mabidi aliyepiga mkwaju kutoka nje ya eneo la kupigia penalti ili kuimarisha matumaini ya timu yake. Mabidi pia aliifungia klabu hiyo mabao yake mawili katika raundi ya kwanza ya mchuano huo wikendi iliopita. Bao hilo lilisababisha mechi hiyo kuwa ngumu ambapo Vita ilionyesha mchezo mzuri ikilinganishwa na wapinzani wao Setif waliojaribu kutumia mbinu chafu za kupoteza muda huku mashabiki wa kilabu hiyo wakitaka kipenga cha mwisho kupulizwa kuanzia dakika ya 75 hadi mwisho.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |