Caf yaipa Morocco tarehe mpya ya mwisho kueleza msimamo wake
(GMT+08:00) 2014-11-04 10:35:29
Shirikisho la Soka la Afrika limesisitiza halitabadilisha tarehe ya michuano Afcon na kuipa Morocco hadi Jumamosi kuamua kama watakuwa wenyeji kama ilivyopangwa. Morocco inataka michuano iahirishwe kutokana na hofu ya mlipuko wa Ebola. Caf imeitaka Morocco iweke wazi msimamo wake hadi Novemba 8, tarehe ambayo pia imepewa nchi yoyote ile itakayokuwa tayari kuchukua nafasi ya uenyeji. Caf imesema uamuzi wa mwisho utatolewa Novemba 11 huko Cairo Misri. Mkutano huo wa Rabat ulipangwa mwezi uliopita kufuatia Morocco kuiandikia Caf na kuiomba kuahirisha mashindano hayo, baada ya kushauriwa na wizara yake ya afya kwamba kukaribisha timu 16 nchini humo kutasababisha hatari kubwa ya kuenea kwa virusi hivyo hatari, ambavyo vimeshaua takriban watu 5000, wengi wao wakiwa kutoka Afrika. Hata hivyo Caf ilikataa mara moja na kusisitiza kuwa shindano la wiki tatu litaendelea kama lilivyopangwa kuanzia Januari 17 hadi Februari 8.