• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Msomi wa Marekani: Reli ya Tazara ilisaidia kuendeleza vijiji

    (GMT+08:00) 2014-11-04 16:48:14

    Kituo cha kutuma vifurushi kwa njia ya reli ya Tazara. Jamie Monson anasema wakati reli hiyo ilipojengwa kumekuwa na maelfu ya barua na nyaraka nyingi zilizotumwa kwenda vituo mbalimbali

    Dkt Jamie Monson akimhoji mmoja wa wazee wa China aliyekwenda kujenga reli ya Tazara miaka ya 70. Kwa sasa mzee huyo yuko mjini Harbin, mkoa wa Heilojiang, China

    Kunao msemo mmoja wa China unaosema "unapotaka kuwa tajiri,jenga barabara".

    Maana yake ni kuwa bidhaa za mashambani na raslimali nyingine zinaweza kusafirishwa kwenye miji mikuu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali itakayosaida ukuaji wa uchumi wa watu na nchi.

    Baada ya kufahamu umuhimu wa miundo mbinu ya usafiri, wachina wamepiga hatua na kuwa na mojawepo wa njia bora zaidi za reli duniani.

    Lakini mbali na China, serikali ya China imekuwa ikisaidia nchi nyingi za Afrika kuendeleza miundo mbinu yao kwa kujenga barabara na reli.

    Mfano mzuri ni reli ya Tazara inayoziunganisha nchi za Tanzania na Zambia iliyojengwa na wachina miaka ya sabini.

    Kwa macho ya wengi, umuhimu mkubwa wa barabara au reli ni kuunganisha miji mikubwa na kuhimiza biashara kubwa.

    Lakini msomi na mtafiti Dkt. Jamie Monson ambaye amekaa sana nchini Tanzania na Zambia kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu reli ya Tazara ana maoni tofauti.

    "Sehemu nyingi zilikuwa msitu kabla ya reli kujengwa kama vile mlimba nchini Tanzania na watu walikuwa wachache sana lakini sasa pamekuwa na shughuli nyingi za kibiashara na kilimo na sasa ni mji mkubwa. Watu wa jamii ya wasukuma ambao ni wafugaji ng'ombe walifika kule wakati reli ilipojengwa"

    Kufuatia ujenzi wa reli ya Tazara, wakaazi wa vijijini pia walianza kupata huduma za kijamii kwa urahisi kwa sababu ya kuwa na njia ya haraka ya uchukuzi.

    Wakulima na wafugaji waliweza kuwalipia watoto wao karo za shule kwa kuuza kwa wingi bidhaa zao na uchumi wa jumla wa vijijini ulibadilika.

    Watu wa jamii moja walitangamana zaidi na wengine ndani ya treni wanaposafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine na mawasiliano yaliongezeka.

    Huduma ya kutuma mizigo na barua pia ilirahisishwa.

    Wakati akifanya utafiti wake Dkt. Jamie aliwauliza wakaazi jinsi maisha yalivyokuwa kabla ya ujenzi wa reli ya Tazara.

    "Kuna wengine waliniambia kwamba walitembea kwa mguu, walindesha baiskeli ama kutumia mtumbwi kwenye mto wa kilombero na wengine labda waliweza kutumia basi lakini ilikuwa ngumu sana. Uchumi wao ulikuwa mdogo sana. Lakini baada ya reli kujengwa, kitu cha kwanza ni kwamba watu walipata msaada wa kutembea kwa urahisi. Pia watu ambao walikuiwa wanakaa maeneo ya jombe iringa ama mbeya ambako kilimo ni vigumu walitumia reli kutafuta mahali pazuri pa kukaa na kuanza kulima. Watu pia waliweza kununua vitu kwenye mji mkubwa na kuuza kqwenye vijiji vidogo vidogo"

    Wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara China pia haikuwa na uwezo mkubwa wa kiuchumi, lakini walifahamu njia moja ya kukuza uchumi ni kujenga miundo mbinu ya uchukuzi.

    Walipotembelea Beijing mwaka wa 1965, rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere hakutaka kumweleza Rais Liu Shaoqi kwamba anahitaji msaada wa ujenzi wa reli kwa kuwa China wakati huo pia ilikuwa ni nchi maskini.

    Hata hivyo mwenyekiti Mao Zedong alimwambia Nyerere nyinyi watanzania mna matatizo kama sisi lakini matatizo yetu ni tofauti, hivyo tutasitisha ujenzi wa reli yetu ili tuwasaidie kujenga yenu.

    Huo ulikuwa ni mfano wa kuhamisha ndoto ya utajiri kutoka kwa China hadi Afrika.

    Kulingana na Dkt. Jamie, kujitolea kwa wachina wakati huo kujenga reli katika mazingira magumu ilikwa ni ishara ya urafiki wenye lengo la kusaidia kukuza uchumi.

    "wachina walioenda Afrika kutoka hapa China kazi zai zilikuwa ngumu sana wengi walikaa miaka miwili au minne na hawakuwa na familia na wachache tu walipata nafasi ya kurudi. Naweza kusema wale watu walioungana pamoja kujenga reli kwa kweli walifanya kitu cha maana sana. Ukiangalia ujenzi wa reli au ujenzi wa barabara sio kwamba miradi yote ya wachina inasadia kutoa mali afrika na kupeleka kwa wachina"

    Takwimu zinaonyesha kwamba tangu mwezi aprili mwaka jana zambia ilisafirisha zaidi ya tani 15, 000 za shaba hadi katika bandari ya Dar es salaam nchini Tanzania.Hivi sasa uwezo huo unaendelea kupungua kutokana na kuzeeka kwa reli hiyo.

    Hata hivyo matuimani ya kuinua tena uwezo wa reli hiyo ya kilomita 1,860 huenda yakafikiwa baada ya serikali ya China kuahidi kuikarabati.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako