Licha ya video kuonyesha nyota wa Manchester United Marouane Fellaini akimtemea mate Sergio Aguero kwenye mchezo na Manchester City huenda nyota huyo akaepuka adhabu. Kipigo cha bao 1-0 kilikuwa cha nne mfululizo kutoka kwa watani wao wa jadi na kimefanya wachezaji wa Man United wachanganyikiwe huku wengine wakifanya matukio ya ajabu. Ilikuwa ni aibu kwa timu hiyo kwani wameweka rekodi ya mwanzo mbaya katika kipindi cha miaka 28 na huenda jambo hilo ndilo lilifanya timu iwe na mashaka. Lakini kocha wa Man United Louis Van Gaal amemtetea mchezaji wake raia wa Ubelgiji akisema ameona mjadala huo kwenye mitandao ya jamii, lakini video inaonyesha mchezaji wake akipiga kelele, wakati mwingine unapopiga kelele, mate yanaweza kukutoka. Huwezi kusema huko ni kutema mate. Picha zinaonyesha mchezaji huyo akitoa rundo la mate kwenye uso wa Aguero ambaye alikuwa amelala chini. Chama cha Soka England (FA) kitachunguza suala hilo kwa makini lakini pia kuna kila dalili kwamba wanaweza wasitoe adhabu kwa mchezaji huyo iwapo hoja ya kupiga kelele itapitishwa. Hakuna uthibitisho kwamba alimtemea mate kwa makusudi na hiyo ndio inaweza kumwokoa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |