• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Njia ya hariri ya baharini yainua ushirikiano kati ya China na nchi zilizoko kando ya njia hiyo

    (GMT+08:00) 2014-11-11 16:52:08

    Mpango wa kujenga njia ya hariri ya baharini ya karne 21 ulipendekezwa na rais Xi Jinping wa China mwezi Oktoba mwaka jana alipofanya ziara nchini Indonesia. Baadaye mpango huo uliwekwa kwenye ripoti ya kazi za serikali ya China na kuwa mkakati muhimu wa China katika kuhimiza ufunguaji mlango wa pande zote. Maonesho ya njia ya hariri ya baharini ni hatua moja ya kutekeleza mpango huo.

    Maonesho hayo yalifanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 2 Novemba mjini Dongguan, na kuhudhuriwa na watu kutoka nchi na sehemu 42, mashirika 173 ya wafanyabiashara kutoka China na nchi za nje, makampuni zaidi ya 1000 yaliyoonesha bidhaa zao, na makampuni zaidi ya 6000 yaliyoagiza bidhaa. Maonesho hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza, lakini yamepokewa vizuri na makampuni ya China na nchi za nje, ambayo yaliomba mabanda 2,536 ya maonesho, idadi ambayo ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa kwa asilimia 26.8.

    Makampuni kutoka nchi 25 zilizo kando ya njia ya Hariri baharini na nchi 14 zisizo kando ya njia hiyo yalionesha bidhaa zenye sifa ya kipekee kwenye maonesho hayo, zikiwemo mbao za mbambakofi kutoka Laos, vipande vya kamba kutoka Indonesia, matunda kutoka Thailand, na mapambo kutoka India.

    Kwa ujumla watu elfu 80 walitembelea maonesho hayo, na mikataba ya miradi 451 yenye thamani ya yuan bilioni 174.7 ilisainiwa.

    Mfanyabiashara mmoja kutoka Sri Lanka alionesha chai ambayo ni bidhaa ya jadi inayosafirishwa kupitia njia ya hariri baharini kwenye maonesho hayo. Anasema mwaka jana alionesha chai kwenye maonesho ya Asia Kusini huko Kunming, kila siku watu zaidi ya elfu moja walionja chai chake, baadaye watu wengi walimwandikia barua pepe kumwuliza lini atakuja tena China. Jambo hili limemfanya kutambua kuwa China ina soko kubwa kwa bidhaa zake.

    Alisema anajua kuwa rais Xi Jinping wa China anataka kujenga tena njia ya hariri baharini, na maonesho hayo ni hatua moja ya utekelezaji wa mpango wake. Anapenda sana mpango huo, na anaamini kwamba kutokana na fursa hii nzuri, atawapatia wateja wa China chai yenye sifa nzuri, na shughuli zake hakika zitapanuliwa siku hadi siku.

    Waziri wa zamani wa utalii wa Malaysia Bi. Ng Yen Yen alisema mwaka jana Malaysia ilipokea watalii milioni 25, anatarajia kuwa kutokana na ujenzi wa njia ya hariri baharini, Malaysia itapokea watalii milioni 60. Anaona kuwa ujenzi wa njia hii utaunganisha bandari nyingi, hivyo anapendekeza nchi zilizo kando ya njia hii zishirikiane kuendeleza meli za utalii za kiwango cha juu, ambayo italeta faida zaidi ya dola za kimarekani bilioni moja na fursa nyingi za ajira, na kunufaisha uchumi wa nchi mbalimbali.

    Bibi Ng Yen Yen alisema meli za utalii zimepata maendeleo ya kasi zaidi kati ya shughuli nyingine za utalii, na inakadiriwa kuwa ongezeko la shughuli hiyo litaendelea kuinuliwa. Hivi sasa utalii kwa kutumia meli umepata maendeleo zaidi katika nchi za Asia kuliko Amerika ya Kaskazini, na mwaka jana mamia ya meli zilitoa huduma katika nchi za Asia ambazo ziliingiza pato la dola za kimarekani bilioni 2.1. Anaamini kuwa njia ya hariri ya baharini ya karne 21 itaongeza mapato kwa mara kumi zaidi.

    Mwanauchumi maarufu Lin Yifu anaona kuwa nchi zilizo kando ya njia ya hariri zina rasilimali nyingi na vivutio vingi vya utalii, soko lao lina uwezo mkubwa wa kupata maendeleo katika siku zijazo, na gharama ya nguvu kazi ni nafuu. Baada ya msukusuko wa uchumi kutokea mwaka 2008, ongezeko la uchumi wa nchi za Amerika ya Kaskazini na Ulaya umepungua, hivyo nchi zilizo kando ya njia ya hariri baharini zenye maendeleo madogo na mustakabali mzuri ni soko jipya kwa makampuni ya China.

    Wataalamu na wafanyabiashara walioshiriki kwenye maonesho hayo wanaona kuwa, kutokana na utekelezaji wa mkakati wa kujenga njia ya hariri ya baharini ya karne 21, China, nchi za ASEAN na nchi nyingine zilizo kando ya njia hii huenda zitapata maendeleo makubwa zaidi katika miaka kumi ijayo.

    Mkuu wa kitivo cha uhusiano wa kimataifa na mambo ya umma cha Chuo Kikuu cha Fudan Bw. Long Yongtu anaona kuwa, China itatakiwa kuanzisha utaratibu wa ushirikiano ili kutimiza mkakati wa kujenga njia ya hariri ya baharini. Hatua ni pamoja na kuanzisha kamati ya ushirikiano inayoshirikiwa na nchi nyingi na kuanzisha sektretarieti.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako