Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) linahangaika kusaka mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Chalenji mwaka huu yaliyopangwa kuanza mwishoni mwa Novemba. Awali, mashindano hayo ya kila mwaka yalipangwa kufanyika Ethiopia, lakini hivi karibuni chama cha soka cha nchi hiyo kiliijulisha Cecafa kuwa hakitaweza kuandaa mashindano hayo baada ya kutoungwa mkono na Serikali. Kwa mujibu wa Cecafa ingawa Ethiopia imejitoa hii haimaanishi kuwa mashindano hayatafanyika, na hivi sasa wamefanya mazungumzo na Sudan, ila kesho Jumamosi ndio itajulikana mbichi na mbivu kama wamekubali au la, ambapo ikikataa Cecafa itaiomba nchi nyingine. mashindano hayo huenda yatasogezwa mbele na kwamba yanaweza kuanza Desemba. Cecafa imeongeza kuwa wakipata nchi ambayo itakuwa tayari kuandaa mashindano ndipo watapanga ratiba, lakini mpaka sasa tarehe rasmi ya mashindano bado haijapangwa na kusisitiza kuwa lazima mashindano yasogezwe mbele ili kutoa nafasi ya maandalizi kwa nchi itakayoyandaa. Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Kenya wana shauku ya kutetea taji lao, ila watakutana na ushindani kutoka kwa mabingwa mara 13, Uganda, Sudan na hata Ethiopia.
| © China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |