Kocha wa zamani wa Yanga, Tom Saintfiet amefukuzwa kazi na klabu yake ya Free State Stars ya nchini Afrika Kusini baada ya timu yake kufungwa mechi tano kati ya 10 alizokuwa benchi. Saintfiet aliifundisha Yanga 2012 na kuipatia Kombe la Kagame kabla ya kutimuliwa baada ya mechi tatu pekee za Ligi Kuu msimu huo Yanga ilipofungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar. Kocha huyo ametimuliwa baada ya timu yake kufungwa mabao 5-2 na Polokwane City nyumbani Jumanne ya wiki iliyopita. Kwa ujumla Saintfiet aliiongoza timu yake kushinda michezo mitatu, sare mbili na kupoteza michezo mitano jambo ambalo limewakasirisha viongozi wa timu hiyo. Awali Kocha mwingine wa zamani wa Yanga, Kosta Papic naye alitimuliwa na timu ya Chippa United aliyokuwa akiifundisha nchini humo. Makocha hao wote wameonekana hawana mpya. Saintfiet alitaka kumsajili Ngassa Agosti mwaka huu lakini dili hilo lilishindikana baada ya Yanga kugoma. Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Azam FC mwaka huu wa 2014 hivi sasa wako mbioni kumsajili beki wa Ivory Coast, Pascal Serge Wawa toka klabu ya El Mereikh ya nchini Sudan. Wawa ambaye ana umri wa miaka 28 ni beki ambaye amewahi kuichezea timu ya taifa ya Ivory Coast kwa wachezaji wenye umri chini miaka 23 ambapo alishiriki michuano ya kimataifa kwa vijana inayofanyika kila mwaka nchini Ufaransa na pia amewahi kufanya majaribio kwenye timu ya ligi kuu ya Ufaransa ya Lorient.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |