Real Sociedad yampa jahazi David Moyes kuliongoza
(GMT+08:00) 2014-11-12 10:23:50
Kocha wa zamani wa timu ya Manchester United David Moyes ametajwa rasmi kuwa kocha mpya wa klabu inayoshiriki ligi ya Hispania, Real Sociedad. Kocha huyo mwenye miaka 51, hii ni kazi yake ya kwanza baada ya kutimuliwa kwenye klabu ya Man U mwezi wa nne mwaka huu na kuwa nje ya mchezo wa soka bila ajira yoyote kwa miezi 10. Moyes ambaye anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jagoba Arrasate aliyetimuliwa na Sociedad baada ya matokeo mabaya na kusababisha timu hiyo kuangukia nafasi ya 15 katika ligi kuu nchini humo, maarufu kama La Liga amepewa mkataba wa miezi kumi na nane sawa na mwaka mmoja na nusu. Mkataba wa Moyes na Real Sociedad ni mpaka june mwaka 2016 na kwa mara ya kwanza ataonekana katika mechi ya Deportivo November 22. David Moyes alichukua takribani wiki moja kabla ya kufikia uamuzi wa kuichukua klabu hiyo japo alishindwa katika jaribio lake la kumshawishi beki wa zamani wa Manchester United Phil Neville kuungana naye kama msaidizi wake. Moyes ambaye ni raia wa Scotland anakuwa kocha wa tatu toka visiwa vya Ufalme Wa Uingereza yaani United Kingdom kuwa kocha wa klabu hii ya Real Sociedad waliopita kabla yake wakiwa John Tosha na Chirs Coleman wote wakitokea Wales.