• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Eneo la uzalishaji wa nafaka nchini China lakumbwa na tatizo linalosababishwa na uteketezaji wa mabua

    (GMT+08:00) 2014-11-26 18:04:23

    Eneo la kaskazini mashariki mwa China lina ardhi yenye rutuba nyingi, na ni kituo kikubwa zaidi cha uzalishaji wa nafaka nchini China. Wakati eneo hili linapopata mavuno makubwa kwa miaka mingi mfulululizo, pia limekabiliwa na tatizo linalosababishwa na uteketezaji wa mabua. Wataalamu wanaona kuwa, matumizi ya mabua ni mahitaji ya dharura katika eneo hilo, kutumia mabua kama nishati huenda kutakuwa mwelekeo wa siku zijazo.

    Hivi karibuni mikoa ya Heilongjiang, Jilin na Liaoning ilikumbwa na hewa chafu yenye vumbi jepesi la pm2.5, ambayo pia iliathiri miji mingi mikubwa ikiwemo Harbin, Changchun, Shenyang. Uteketezaji wa mabua ni sababu kubwa ya uchafuzi huo.

    Kwa mujibu wa ripoti ya ubora wa hali ya hewa iliyotolewa na mji wa Changchun, mwishoni mwa mwezi uliopita, kiasi cha vumbi jepesi la pm2.5 kwenye mita moja ya ujazo ya hewa kilikuwa microgram 605, faharisi ya ubora wa hewa AQI ilikuwa 500, ambayo ni uchafuzi mkubwa sana. Mkazi wa mji wa Changchun Bw. Zhang Guo alisema uchafuzi kutokea wakati mvua inaponyesha si jambo linalotokea mara kwa mara, zamani mji huo ulikuwa na hewa nzuri, na hafahamu kwa nini hali hii imebadilika.

    Serikali ya China inaunga mkono matumizi ya mabua badala ya uteketezaji wake. Baraza la serikali la China limetoa maoni kuhusu kuharakisha matumizi ya mabua, na kamati ya maendeleo na mageuzi ya China ilitoa mpango wa matumizi ya mabua katika kipindi cha 12 cha miaka mitano ya maendeleo ya uchumi na jamii, na mikoa mingi iliyoko kaskazini mashariki inatafiti njia za kutumia mabua.

    Takwimu zilizotolewa na kamati ya kilimo ya Changchun zinaonesha kuwa uzalishaji wa mabua mjini humo ni tani milioni 12 hadi 13. Mabua yanaweza kusagwa kisha kutumiwa kwa kuchoma au kwa kuzalisha umeme.

    Mkurugenzi wa ofisi ya uratibu wa shughuli ya kamati ya maendeleo na mageuzi ya mji wa Changchun Bw. Jiang Yi anasema, mji huo ulianza kutafiti matumizi ya mabua mwaka 2011, na mradi wa kampuni ya Dacheng wa kuzalisha sukari inayotumiwa viwandani kwa mabua ndio mmoja kati ya miradi mikubwa ya matumizi ya mabua.

    Habari zinasema, sukari inayozalishwa na kampuni hiyo kwa mabua si kama tu ina bei nafuu, bali pia ina ubora mzuri. Kuzalisha tani moja ya sukari kunahitaji tani 2.5 tu za mabua ya mahindi. Wakulima wakizalisha tani moja ya mahindi, wanaweza kupata yuan 960 kutokana na mauzo ya mabua.

    Lakini matumizi ya mabua bado yanakabiliwa na matatizo mbalimbali. Kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo ukusanyaji na usafirishaji, na baadhi ya wakulima kuuza mabua kwa bei kubwa kupita kiasi, baadhi ya makampuni ya nishati ya viumbe na viwanda vya kuzalisha umeme haviwezi kupata mabua ya kutosha kwa bei mwafaka, na vimesimamisha kazi zinazotumia mabua.

    Miji mbalimbali ya mikoa ya kaskazini mashariki mwa China imezitaka idara husika kutafiti njia ya kuinua ufanisi wa matumizi ya mabua, na kutoa uungaji mkono wa kisera na kifedha kwa shughuli za kutumia mabua kuzalisha umeme, karatasi, na malisho ya mifugo, pia kuongeza utoaji wa ruzuku kwa wakulima ili kuwahimiza kutumia mabua kuwa mbolea.

    Mkurugenzi wa ofisi ya sera na sheria ya kamati ya kilimo ya Changchun Bw. Kong Lingbo anaona kuwa, China bado iko kwenye kipindi cha kwanza katika matumizi ya mabua. Anapendekeza serikali kuu kutoa sera nyingi zaidi kuhusu kutoa ruzuku ya ununuzi wa mashine za kutengeneza mabua, kuongeza matumizi ya mabua viwandani, na kuwahimiza wakulima kutumia mabua kuwa mbolea.

    Wataalamu wanaona kuwa matumizi ya mabua viwandani ni njia itakayotatua kabisa uchafuzi wa hewa unaosababishwa na uteketezaji wa mabua. Idara husika zinatakiwa kuchukua hatua halisi kutatua matatizo ya kutumia mabua.

    Ili kuzuia athari mbaya ya uteketezaji wa mabua kwa ubora wa hewa, harakati za kupiga marufuku kuteketeza mabua zimetekelezwa katika sehemu mbalimbali. Lakini baada ya harakati hizi kuanza, baadhi ya wakulima hawateketezi mabua muda wa mchana, wanayateteteza kisirisiri wakati wa usiku, hivyo baadhi ya mikoa pia ilianza kufanya ukaguzi usiku.

    Mkoa wa Jilin umeamua kutoa ripoti kuhusu uteketezaji wa mabua kila baada ya siku tatu, na kutuma vikundi vya ukaguzi katika sehemu mbalimbali kudhibiti uteketezaji wa mabua. Idara ya uhifadhi wa mazingira ya mkoa huo imezitaka idara za uhifadhi mazingira za ngazi mbalimbali ziimarishe usimamizi, na kushirikiana na idara za misitu, kilimo, polisi na kamati ya maendeleo na mageuzi kufanya ukaguzi kwa makini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako