• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano wa 9 wa wakuu wa kundi la G20 wamalizika

    (GMT+08:00) 2014-11-16 20:28:39

    Mkutano wa 9 wa siku mbili wa wakuu wa kundi la G20 umemalizika mjini Brisbane, Australia. Ajenda kuu tatu za mkutano huo zilizowasilishwa na Australia kama mwenyekiti wa zamu wa kundi hilo ni pamoja na kuhimiza ukuaji na kutoa nafasi za ajira, kuimarisha nguvu na uhai wa uchumi wa dunia na kuboresha mashirika ya kimataifa.

    Mkutano huo umetoa taarifa ya pamoja na kupitisha Mpango wa Utekelezaji wa Brisbane, na kutoa hatua elfu moja za kuhimiza ukuaji wa uchumi wa dunia, kuongeza nafasi za ajira na kusukuma mbele mchakato wa biashara huria.

    Kuhusu kuhimiza ukuaji na ajira, viongozi wa G20 wamekubaliana kutenga fedha zaidi katika sekta ya miundo mbinu.

    Hivi sasa, uchumi wa Marekani umeanza kufufuka upya, huku uchumi wa China ukidumisha ukuaji wa asilimia 7, na nchi hizo mbili zinachukuliwa kuwa nguvu muhimu za kufufua na kuhimiza ukuaji wa uchumi duniani. Rais Barack Obama wa Marekani amesema nchi yake na China zinaendelea kupanua ushirikiano. Amesema Marekani na China zimefikia makubaliano ya kuongeza muda wa visa za biashara, utalii na masomo, jambo ambalo litahimiza maendeleo ya sekta ya utalii na biashara ya nchi hizo mbili na kutoa nafasi za ajira zaidi. Amesema Marekani na China pia zimekubaliana kusaini makubalianao ya uwekezaji wa pande mbili, na makubaliano ya ushirikiano wa teknolojia ya habari yanayojadiliwa na nchi hizo mbili pia yatatoa nafasi za ajira elfu 60 kwa Marekani.

    Kwa muda mrefu, suala la biashara huria limejadiliwa kwenye mikutano ya kundi la G20. Katika mkutano wa mwaka huu, viongozi hao wamekubaliana kuwa kupanua biashara duniani kutazipatia manufaa ya moja kwa moja nchi mbalimbali na wananchi wake.

    Viongozi wa kundi la G20 pia wamejadili hatua halisi za kuimarisha utulivu wa mambo ya fedha na kukubali kupambana na vitendo vya ukwepaji wa kodi vinaovuka mipaka ya nchi kwa kupitia ushirikiano wa kimataifa katika mambo ya kodi ili kuhakikisha kila nchi inapata mapato ya kodi. Katika sekta ya uongozi wa dunia, viongozi hao wamesema mageuzi yanatarajiwa kufanywa kwenye mashirika ya kimataifa ya fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya uchumi wa dunia. Mkutano huo pia umeitaka Marekani iidhinishe kwa haraka hatua za mageuzi kuhusu mgao wa nchi wanachama wa Shirika la Fedha Dunia(IMF) katika shirika hilo.

    Aidha, suala la mabadiliko ya hali ya hewa pia imeandikwa kwenye taarifa ya pamoja.

    Imefahamika kuwa China itakuwa nchi mwenyeji wa mkutano wa kundi la G20 wa mwaka 2016.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako